Tunaponunua kitu, huwa tunaangalia gharama tunayoingia kwenye kununua kitu hicho wakati wa matumizi. Hivyo kama gharama tunaweza kuimudu, tunanunua.

Kuna gharama za msingi na muhimu zaidi kuangalia kuliko ile tu ya kununua. Gharama hizo ni zile endelevu, ambazo zinaambatana na kitu ulichonunua.

Kwa vitu vilivyo wazi kwa gharama zake, huwa tunahesabu wazi. Mfano unaponunua gari, unajua kabisa kuna gharama za kuweka mafuta, gharama za matengenezo na nyinginezo. Ndiyo maana unaweza kuwa na fedha ya kununua gari, lakini usinunue kwa sababu gharama zake endelevu hutaweza kuzimudu.

Lakini kuna vitu vidogo vidogo, ambavyo huwezi kuona gharama zake endelevu.

Mfano maamuzi ya kununua simu janja mpya yenye uwezo mkubwa. Hapo jua unakwenda kuingia gharama za ziada kununua muda wa maongezi na vifurushi vya kuingia mtandaoni. Lakini gharama zaidi itakuwa kwenye muda unaotumia kwenye simu hiyo.

Kadhalika unapojiunga na mtandao wowote wa kijamii, utaambiwa hakuna gharama yoyote ni bure, utashawishiwa kuwa na marafiki au wafuasi wengi zaidi. Na baadaye gharama kubwa inakuja, ambayo ni muda unaotumia kwenye mitandao hiyo, kwanza kutafuta marafiki na wafuasi, baadaye kuendelea kuwasiliana na marafiki hao ili waendelee kuwa na wewe. Unapokuja kukokotoa muda uliowekeza kwenye huduma hizo, unagundua gharama ni kubwa.

Kitu kikubwa cha kuondoka nacho hapa leo ni kabla hujafanya maamuzi yoyote, angalia gharama ambatanishi, gharama zinazoendana na maamuzi hayo, ambazo utaendelea kuingia siku za mbeleni. Zijue mapema gharama hizo ili ufanye maamuzi yaliyo sahihi.

Na usidanganyike kwamba kuna kitu kisicho na gharama za mbeleni. Hata kununuliwa chakula na mtu leo kama zawadi tu, jua kuna gharama itakuja mbeleni. Kuna siku atataka kitu kwako, ambacho hutakuwa tayari kumpa, lakini kwa kuwa alishakununulia chakula huko nyuma, unasukumwa kulipa fadhila. Chakula ni mfano tu, lakini inaweza kuwa zawadi nyingine yeyote ambayo mtu anakupa, na baadaye inakuwa gharama kwako kulipa.

Unapoelewa kila kitu kina gharama za mbeleni, unafanya maamuzi yako kwa usahihi na kuwa tayari kukabiliana na kile kinachokuja.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha