Mpendwa rafiki yangu,
Aliyekuwa mtawala wa Ufarasa na jemidari wa kijeshi Napoleon Bonaparte aliwahi kunukuliwa akisema, niliwavuta watu wangu kwa kutumia mabavu, lakini Yesu aliwavuta watu wake kwa kutumia upendo.
Wako wazazi ambao wanatumia mabavu katika malezi ya watoto wao, na siku zote ukitumia mabavu lazima utawapoteza watoto wako.
Unafikiri kwamba, ukitumia mabavu utaweza kuwanyoosha watoto na kuwa katika mstari kumbe siyo.
Ukitaka kuwafanya watoto wako wame marafiki zako basi wavute kwa upendo na wala siyo mabavu. Upendo utakusaidia kuivuta familia yako na itakuwa familia ya kirafiki kuliko mabavu.
Rafiki yangu mmoja, baba yake alikuwa ni mkali sana, sasa hivi karibuni niliwasiliana na rafiki yangu huyo akaniambia, “baba yangu alikuwa mkali sana kiasi kwamba nilikuwa naogopa hata kumuuliza kitu. Nilikuwa napitia changamoto mbalimbali lakini nafikiria ni namna gani nitaweza kumwambia.
Laiti kama baba asingekuwa mkali angenisaidia sana kupata ushauri na kunipa miongozo mbalimbali ya maisha.”
Huyo ni rafiki yangu ambaye anakiri wazi, ukali wa baba yake ulikuwa kikwazo kwake.
Ni watoto wangapi leo wanapitia hali kama hii ya rafiki yangu? Ni wengi sana.
Wazazi wakali kupitia kiasi, wanakuwa wanajenga hofu kwa watoto, watoto wanashindwa kuwaelezea wazazi wao yale wanayopitia kwa sababu wanajua hata wakiwaeleza wazazi wao ni wakali hivyo hawataweza kusaidika.
Kwa njia ya upendo tutaweza kujenga mahusiano bora kwa watoto wetu lakini pia tutaweza kuwafanya watoto wetu kuwa marafiki zetu.
Mzazi akishakuwa na upendo mtoto atafaidi vingi kwani upendo huvumilia yote. Upendo husikiliza lakini mabavu au ukali kamwe hausikilizi.
Ukitaka ujifunze vitu vingi kwa mtoto wako naye ajifunze vingi kutoka kwako kuwa mzazi rafiki. Jenga naye urafiki kiasi kwamba hata kama anashida anayopitia lazima atakuambia kwa sababu anajua ni rafiki yake utamsikiliza.
Tunapokuwa tuko na rafiki tunakuwa huru kujiachia na kumwambia chochote kile tunachojisikia kwa sababu tunajua ni rafiki. Hata sisi tunapokuwa na watoto tujitahidi kuishi maisha ya kirafiki tutawafanya watoto wetu kuwa bora sana.
Mzazi rafiki anajenga uhuru kwa mtoto wake, uwezo wa kujiamini na kuthubutu kufanya makubwa kwa sababu anajua hata akikosea au akipata yuko rafiki yake ambaye ni mzazi wa kumtia moyo.
Muda mwingine watoto wanashindwa kuthubutu kwa sababu ya hofu waliyokuwa nayo kutoka kwa wazazi wao. Ukali kwa mzazi unachangia kuua hata vipaji vilivyojificha kwa mtoto.
Hatua ya kuchukua leo; Wazazi jengeni urafiki na watoto wenu.
Wavuteni watoto kwenu kwa njia ya upendo.
Mzazi punguza ukali wa kupitiliza, kuna wakati unatakiwa uweke ukali pembeni na uvae uso wa kirafiki na mtoto wako kwa njia hii utaweza kumjenga mtoto na kuwa bora sana.
Kwahiyo, unao wakati wa kubadilisha mtindo wa malezi badala ya kuwalea watoto kimabavu anza sasa kuwavuta kiupendo na ukishawavuta kiupendo ishi nao maisha ya kirafiki.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.
Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog ,vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana