Kama kuna kitu ambacho ni sharti ukifanye, basi huna uhuru wa kuchagua, unapaswa kufanya. Kuigiza kama vile una uhuru wa kuchagua ni kujidanganya na kujitengenezea msongo zaidi.

Kama una uhuru wa kuchagua kile unachofanya basi hilo siyo sharti, unachagua nini ufanye. Kuigiza kama vile ni sharti kufanya ni kujinyima uhuru uliopo.

Watu wengi wamekuwa wanajidanganya kwenye maeneo hayo mawili na kuishia kufanya vitu kwa namna isiyo sahihi.

Kabla hujafanya chochote, jiulize kwanza kama ni sharti kufanya au kama ni chaguo lako. Kama jibu ni sharti basi fanya unavyopaswa kufanya na usiigize unaweza kuchagua. Na kama jibu ni kuchagua, basi kuwa huru kufanya uchaguzi ulio bora na kufanya kilicho sahihi.

Ni mambo machache sana ambayo ni sharti kwako kufanya, hayo ni yale ya msingi kabisa. Lakini mengi ambayo kwako ni sharti kufanya, umejiingiza kwenye mtego wa aina hiyo mwenyewe. Mfano kama upo kwenye kazi usiyoipenda na umechukua mkopo ambao utaulipa kwa miaka mingi, kufanya kazi hiyo ni sharti kwako, lakini sharti hilo umelitengeneza mwenyewe.

Lengo lako kwenye maisha ni kuwa huru, kupunguza masharti na kuwa na machaguo kwenye kila unachofanya. Kwa kuwa na uhuru huu, hutafungwa na chochote, utaweza kufanya maamuzi mazuri wakati wowote, kwa sababu hakuna kilicho kufunga.

Kwa kila maamuzi unayotaka kufanya kwenye maisha yako, angalia kama yanakupa uhuru wa kuchagua au yanakufungia kwenye masharti. Ukishagundua ni masharti, achana na maamuzi hayo.

Wengi wameingia kwenye masharti kwa kutokutafakari maamuzi wakati wanayafanya. Wewe umeshajua hili, usikubali tena kuingia kwenye mtego huo.

Mafanikio ya kwanza ni kuwa huru, haijalishi una nini, kama huna uhuru wa kuchagua jinsi unavyotaka maisha yako yaende, huwezi kufurahia mafanikio yoyote uliyoyapata.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha