Mpendwa rafiki yangu,
Binadamu tuna tabia moja ambayo huwa inasababisha watu wengi kurudi nyuma badala ya kwenda mbele.
Siyo tu kwenye mahusiano bali hata mambo mengine pia.
Tabia hiyo ambayo inawarudisha watu wengi nyuma ni mazoea. Watu wengi walio katika maisha ya ndoa wanaishi kimazoea kiasi kwamba mke au mume ana sahau wajibu wake. Ukiwa mke au mume na ukashindwa kuitumia nafasi yako vizuri katika ndoa lazima utazaa matatizo makubwa.
Huwa tunajisahau, tunajidanganya kuwa kwa sababu nimeshafunga ndoa hivyo sipaswi kuangaika sana kwani ameshakuwa wangu. Asili ya binadamu ni kupenda kuona vitu vipya, ukiwa katika mahusiano na unakuwa huna ubunifu yaani kila siku wewe unakuwa vile vile huku ndiyo kuishi kimazoea.
Wewe kama mwanandoa usikubali kuizoea ndoa yako, kila siku ona ndoa yako ni mpya usiizoee hata kidogo, mwone mwenza wako ni mpya kwako usimzoee maana ukishamzoea utamchukulia poa.
Mazoea huwa yanavunja ndoa, usifanye chochote kwa mazoea Kila kitu kifanye kama ndiyo mara yako ya kwanza, na weka kazi pia. Huwa tunajidanganya kuweka kazi kwenye maeneo mengine na kusahau mahusiano yetu ya ndoa. Ndoa ina hitaji kazi kama kazi nyingine.
Usiishi kimazoea, unatakiwa kujifunza kila siku kuishi na mwenzako, kuwa mbunifu kwenye kila eneo la maisha yako ya ndoa. Watu huwa hawachoki ubunifu hata siku moja, bali ubunifu katika ndoa huwa unaleta furaha.
Mpe thamani mwenza wako ambayo haiwezi kuipata sehemu nyingine yoyote ile ila kwako tu, hata akiwa sehemu nyingine ambayo atashawishika na wawindaji akifikiria thamani yako tu anarudi nyumbani.
Chukulia kuwa mke, mume wako ni mteja wako, na ukiangalia kwa sasa biashara ni nyingi na wateja ni wachache na mteja ataweza kudumu kwenye biashara yako kama ukimpatia kile anachokitaka kama ni huduma iwe bora ambayo hawezi kuipata sehemu nyingine yoyote ile.
Utampoteza mteja wako pale ambapo wewe utashindwa kumhudumia kwa kumpa thamani kubwa ambayo hawezi kuipata sehemu nyingine yoyote ile.
Unajua kila mtu ana njaa yake katika ndoa? Je unaijua njaa ya mke wako Au mume wako? Utaijuaje sasa njaa ya mwenza wako ili uweze kumshibisha mwenza wako ili asiende kula vyakula vya wengine?
Kipo kitabu kitakachoweza kukupa mwongozo wote huo, ni kitabu cha ijue njaa ya Wanandoa, na kipate sasa kwa kutumia link hii mara moja.
Ingia Hapa; https://www.getvalue.co/home/product_details/ijue_njaa_ya_wanandoa
Kitu pekee ambacho wanandoa huwa wakifanyi ni tathimini. Wanandoa wengi hawakai chini na kutathimini kwa pamoja maisha yao ya ndoa yakoje.
Hivi usipofanya tathimini ya ndoa yako utawezaje kujua kama unaenda mbele au unarudi nyuma?
Maisha ambayo hayatathiminiwi ni maisha ambayo hayana maana kuishi alisema mwanafalsafa Socrates, nami nasema, maisha ya ndoa ambayo hayatathiminiwi ni maisha ambayo hayana maana kuishi.
Kaeni chini, mjichunguze vipi kuhusu mwenendo wenu, unanionaje kwa sasa, wapi siende vizuri unafikiri tufanye nini ili tuwe bora.
Ni ujinga kwa mwanandoa kupata muda wa kutembelea mtandao wa kijamii lakini unakosa muda wa kukaa na mwenza wako hata wa kuongea na kujitathimini.
Kila inapofika kumbukizi ya ndoa yenu, jifanyieni tathimini juu ya ndoa yenu, na kwenye tathimini mnatakiwa mseme ukweli ili muweze kuwa huru.
Ukiigiza kwa kusema ukweli hamtoweza kusaidiana vizuri.
Ukitaka ndoa yako iwe vizuri, jipeni muda wa kujitathimini wa yale mnayofanya.
Shida kubwa wanandoa wengi wanaishi maisha ya ubinafsi ndani ya ndoa. Maisha ambayo hayana umoja na shetani wa ndoa nyingi ni ubinafsi wa wanandoa.
Kwenye ndoa huna chako, bali mna chenu. Ukishaingiza ubinafsi katika ndoa shetani wa ubinafsi ataendelea kuwatafuna.
Hatua ya kuchukua leo;
Usiishi kimazoea katika ndoa yako kila wakati kuwa mbunifu ili msichokane na muone mwenza wako mpya wala usimzoee kiasi cha kumchukulia poa.
Jueni maendeleo ya ndoa zenu kwa kukaa chini na kufanyiana tathimini. Bila kufanyiana tathimini mtakuwa mnaishi maisha ambayo hayana maana kuishi.
Kwahiyo, kila mmoja ataweza kumvuta mwenza wake kwa upendo na siyo mabavu, katika kujenga ndoa unatakiwa kuwa mvumilivu na kuchukuliana.
Huwezi kumbadili mwenzako kwa mabavu bali kwa upendo na itachukua muda kidogo lakini utafanikiwa.
Ukikazana kumbadilisha mtu ndiyo unampoteza anaendelea kukazia tabia aliyekuwa nayo. Anza kujibadili wewe, kupitia wewe, utamvuta kwa maisha yako na wala usitumie nguvu, bali tumia nguvu kujibadili wewe mwenyewe.
Makala hii imeandikwa na
Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali.
Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa
http://kessydeo.home.blog ,vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI. Karibu sana.
Ukawe na siku bora sana rafiki.
Rafiki na mwalimu wako,
Mwl, Deogratius kessy
0717101505//0767101504
deokessy.dk@gmail.com //
Asante sana