Utulivu umekuwa ni kitu kigumu kwenye zama tunazoishi sasa.

Maelewano pia yamekuwa siyo mazuri.

Hali hizi zinachochewa na magumu matatu ya kiroho ambayo wengi wanayapitia kwenye zama tunazoishi sasa.

Ugumu wa kwanza ni kuwapenda wale wanaokuchukia. Ni rahisi kusema adui mpende, lakini inapotokea mtu amefanya jambo linalokukwaza, kukuumiza au kukuangusha, siyo rahisi kujibu kwa upendo. Utaona kufanya hivyo ni kutokujijali, ni kutokumwajibisha na kuwaruhusu wengine wavuruge maisha yako.

Ugumu wa pili ni kuwajumuisha wale waliotengwa, hasa ambao unatofautiana nao kwa namna fulani. Ni rahisi kwenda na wale unaokubaliana nao, kimtazamo na mengine, lakini wale ambao mnapingana, huwa wanaonekana kama maadui. Lakini hao ni watu ambao pamoja na utofauti wao, watakuonesha vitu ambavyo huwezi kuviona wewe mwenyewe. Kumjumuisha mtu ambaye amekuwa anakupinga ni kugumu, lakini kuna manufaa makubwa.

Ugumu wa tatu ni kukubali umekosea. Kila mtu huwa anafanya makosa, lakini kukubali makosa, ni kitu ambacho kwa wengi siyo rahisi. Wengi huona kufanya hivyo ni kukiri udhaifu, kuharibu kile ambacho wamejenga kwa nje. Lakini hakuna kitu chenye manufaa kama kukiri umekosea, kwa sababu unakuwa mnyenyekevu, unajifunza na wengine wanakuamini pia.

Kuvuka magumu haya, chagua kuweka kazi kwenye ukuaji wako wa kiroho. Anza kwa kuwa mwema na kuwa na upendo kwa kila mtu na kila jambo. Mtu anapokosea, kukuumiza au kukukwaza, usiangalie zaidi alichofanya, bali jiweke kwenye viatu vyake, utaona kuna kitu anapitia ambacho hata wewe ungekuwa unapitia, usingetofautiana naye.

Kwa chochote unachofanya, tafuta mtu anayetofautiana na wewe, anayekupinga au kukukosoa kisha mshirikishe, mjumuishe. Kwa yale anayoona tofauti, yatakusaidia wewe kuyaona makosa mapema.

Na mwisho, unapokosea, kiri kosa, na usitoe sababu au visingizio, bali eleza utafanya nini kurekebisha kosa hilo au kuzuia lisijirudie, kisha fanya ulichoahidi.

Kwa kuzingatia maeneo haya matatu, utakuwa na maisha bora, tulivu kwa kuwa na ukomavu wa kiroho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha