Umeamka asubuhi, hujapangilia siku yako itakwendaje, unaona uingie mtandaoni kidogo au ufuatilie habari.
Huko unakutana na habari moto moto, kuhusu msanii aliyefanya jambo la ajabu au mwanasiasa aliyetoa kauli ya hovyo au habari mpasuko za kusisimua.
Siku yako nzima inaendeshwa na habari ulizosikia, unabishana, kupinga au kukubaliana na habari husika kulingana na upande ulichoagua.
Hivyo rafiki yangu ndivyo wengi wanavyoendesha maisha kwa akili za kushikiwa.
Naziita akili za kushikiwa kwa sababu mtu unakuwa hujafanya maamuzi hayo mwenyewe, badala yake unakuwa umeshawishiwa na wengine.
Kwa sasa watu wanaishi kipropaganda zaidi kuliko kimkakati.
Kuna watu wachache wanaoamua nini kizungumziwe kwenye vyombo vya habari na nini kisambae kwenye mitandao ya kijamii.
Unaweza kuona ni haki yako kuwa na maoni kwenye mambo mbalimbali yanayoendelea, lakini jua kuna watu wanayatengeneza makusudi ili kukuchochea wewe uwe na maoni na kukuondoa kwenye yale ya msingi kabisa.
Lengo lako kuu linapaswa kuwa huishi maisha yako kwa akili za kushikiwa, kwa namna yoyote ile, pambana kuishi kwa misingi yako.
Sehemu nzuri ya kuanzia ni kuwa na utaratibu wa kuiishi siku yako, ambao hauathiriwi na chochote kinachoendelea. Yaani kila siku kuna vitu ambavyo lazima uvifanye, ili unapoimaliza siku yako, unajua kuna ushindi umepata.
Pia epuka kuanza siku zako kwa kufuatilia habari au mitandao ya kijamii badala yake ianze kwa kujifunza maarifa ambayo yanakusaidia kufika kule unakokwenda.
Epuka maoni ya watu kama sumu yenye madhara makali, badala yake utafute ukweli. Maoni ni rahisi, kila mtu anayo, lakini kitakachokusaidia wewe siyo maoni, bali ukweli.
Kwa kila maamuzi unayofanya, jiulize kama umeyafanya kwa kufikiri mwenyewe au kwa akili za kushikiwa.
Kama umekasirishwa na kile ambacho kinaendelea kwenye habari au mtandaoni, jiulize ni akili zako zinakufanya ukasirike au akili za kushikiwa.
Akili za kushikiwa ndiyo chanzo cha matatizo na changamoto nyingi ambazo watu wanazipitia. Ukiweza kuondokana na akili hizo, ukajipa njia ya kufikiri kwa akili zako, utapunguza changamoto nyingi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,