“Unqualified activity, of whatever kind, leads at last to bankruptcy.” – Johann Wolfgang von Goethe

Adui wa kwanza wa mafanikio yako ni wewe mwenyewe.
Kikwazo kikubwa kwako kupiga hatua kwenye maisha, ni mambo ambayo unayafanya sasa.
Kule unakopeleka nguvu zako, muda wako na umakini wako ndiko kunakopelekea wewe kubaki hapo ulipo sasa.

Malalamiko ya kila mtu ni muda hautoshi, mambo mengi muda mchache.
Wengine wakilalamikia uchovu na kusongwa na mengi.

Tunachopaswa kujua ni kwamba, kuna mambo machache mno ambayo tukiweka nguvu na umakini wetu, tutaweza kufanya makubwa.
Lakini tunahangaika na mengi,
Tunatawanya nguvu zetu kwenye mambo mengi,
Na mengi kati ya hayo siyo muhimu kabisa.

Kinachokuangusha na kukurudisha nyuma ni yale unayofanya sasa.
Huna muda kwa sababu unaendekeza mambo yasiyokuwa na umuhimu wowote kwako.

Asubuhi ya leo tafakari kila ambacho umekuwa unafanya,
Angalia kwa wiki moja na kagua kila ulichofanya,
Kisha angalia katika yote uliyofanya, yapi ambayo yanakufikisha unakoenda na yapi hayakufikishi.
Yanayokufikisha ndiyo yanastahili muda wako.
Yasiyokufikisha ni usumbufu kwako, ndiyo kikwazo kwako.
Hatua ya kuchukua ni kuacha kuyafanya mara moja.

Unakwama kwa sababu unahangaika na mambo mengi yasiyo na umuhimu kwako.
Anza kupunguza mambo unayofanya na utaona matokeo makubwa kwenye yale machache unayoyapa muda wako wote, akili zako zote, umakini wako wote na nguvu zako zote.
Usijitawanye kwenye mengi, bali jikusanye kwenye machache.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu akili za kushikiwa, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/09/08/2078

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.