Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu cha GIVE AND TAKE; A Revolutionary Approach to Success kilichoandikwa na Adam Grant.

Kitabu hiki kinaelezea njia ya kimapinduzi ya kutuwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.

Kwa miaka mingi, mafanikio yamekuwa yanaonekana ni zao la mtu kuwa na hamasa, kupenda anachofanya, kuweka juhudi kubwa, kuwa na kipaji na kukutana na bahati. Lakini kwa zama tunazoishi sasa, ambapo mabadiliko ni makubwa, mafanikio yanategemea zaidi jinsi tunavyojihusisha na watu wengine.

Kwenye kitabu hiki cha GIVE AND TAKE, mwandishi ameonesha kinachowapandisha au kuwashusha watu kwenye mafanikio, inategemea zaidi anajihusishaje na watu wengine inapokuja kwenye kutoa na kupokea.

Kupitia tafiti na hadithi za watu mbalimbali waliofanikiwa sana, mwandishi ameweza kuona mahusiano ya aina tatu ambayo watu wanakuwa nayo;

Aina ya kwanza ni kupokea au kuchukua, hawa mwandishi anawaita TAKERS. Hawa ni wale ambao wanachukua zaidi kwa wengine kuliko wanavyotoa. Kwa nje watu hawa huonekana ndiyo wanaofanikiwa, na hata mtazamo kwenye jamii ni kwamba wale waliofanikiwa zaidi basi wamechukua zaidi kwa wengine. Lakini kupitia tafiti na hadithi za mafanikio, mwandishi anatuonesha hawa huwa wanashindwa vibaya na hata wakifanikiwa mwanzoni, mwisho wanakuja kuanguka.

Kundi la pili ni wale ambao mahusiano yao ni ya nipe nikupe, hawa mwandishi anawaita MATCHERS. Watu hawa huwa wanatoa lakini kadiri ya wanavyopokea kwa wengine. Wakitoa kitu kwa mtu, ni kwa sababu wanategemea kupata kitu fulani. Kabla hawajatoa wanaangalia kama wanayetaka kumpa amewahi kuwapa kitu au anaweza kuwapa kitu baadaye. Kupitia tafiti na mifano, mwandishi atatuonesha kwamba watu wa aina hii huwa hawafikii mafanikio makubwa na wala pia hawaanguki kabisa. Hawa huwa wanaishia katikati.

Kundi la tatu ni la watoaji, ambao mwandishi anawaita GIVERS. Hawa ni watu ambao kwenye mahusiano yao na wengine, huwa tayari kutoa zaidi ya wanavyopokea. Wao wanatoa bila ya kuangalia wanapata nini. Kwa mwonekano wa nje, watu hawa huchukuliwa kuwa wanaoshindwa, kwa sababu utayari wao wa kutoa unawafanya wengine wajinufaishe kupitia wao, huku wakiwa hawalipi fadhila zao. Lakini kupitia tafiti na hadithi za waliofanikiwa, mwandishi anatuonesha kwamba wale wanaofanikiwa sana na mafanikio yao kudumu, huwa ni watoaji.

Kitu kikubwa tunachokwenda kujifunza kwenye kitabu hiki ni kwamba ili ufikie mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unapaswa kuwa mtoaji, utoe bila kuangalia unapata nini. Lakini hapo pia kuna tahadhari, kama ambavyo mwandishi atatuonesha, baadhi ya watoaji wamekuwa wanashindwa kabisa, kwa sababu ya mtazamo walionao. Hivyo tunajifunza aina ya utoaji ambayo itatuwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye chochote unachofanya.

Kitabu hiki kimesheheni tafiti mbalimbali za kisaikolojia, kijamii na kiuchumi ambazo zimewahi kufanywa na kuonesha matokeo katika watu wa aina hizo tatu. Pia mwandishi ametupa mifano ya watu waliofanikiwa sana na wengine walioshindwa kutokana na upande wa mahusiano walipo.

Hiki ni kitabu ambacho kila anayetaka mafanikio makubwa anapaswa kukisoma na kuiishi misingi yake kwenye maisha, kitu ambacho kitampa mafanikio makubwa na utulivu wa maisha.

Kuhusu mwandishi.

Adam M. Grant (kuzaliwa Agosti 13, 1981) ni mwanasaikolojia wa nchini Marekani na mwandishi wa vitabu mbalimbali. Adam pia ni profesa wa saikolojia kwenye chuo kikuu cha Pennsylvania shule ya Wharton, akibobea zaidi kwenye saikolojia ya mashirika.

Adam alipata uprofesa wake akiwa na umri wa miaka 28, akiwa mtu pekee kuwahi kupata uprofesa kwa umri mdogo kama wake kwenye shule ya Wharton

Adam ameandika vitabu mbalimbali kama Give and Take: A Revolutionary Approach to Success (2013), Originals: How Non-Conformists Move the World (2016) na Option B: Facing Adversity, Building Resilience, and Finding Joy (2017).

Adam pia ni mnenaji na mshauri wa mashirika mbalimbali kwenye eneo la saikolojia. Unaweza kufuatilia zaidi kazi zake kupitia tovuti yake ambayo ni; www.adamgrant.net

Karibu kwenye uchambuzi.

Kitabu hiki kina sehemu nne, utangulizi, sehemu ya kwanza, ya pili na hitimisho.

Kutakuwa na chambuzi nne za kitabu kama zilivyo sehemu za vitabu. Hivyo karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki, tujifunze njia mpya na ya kimapinduzi ya kufikia mafanikio makubwa kwa kuwa mtoaji.

Unayokwenda kujifunza kwenye kitabu.

Kitabu hiki cha GIVE AND TAKE kinakwenda kuweka mkazo kwenye manufaa ya utoaji kwenye mafanikio. Lakini pia kitaonesha nyakati ambapo utoaji unakuwa kikwazo kwa baadhi ya watu.

Sehemu ya kwanza ya kitabu tunajifunza misingi mikuu minne ya utoaji ambayo ni MTANDAO, KUSHIRIKIANA, KUTATHMINI na KUSHAWISHI.

Tutaona jinsi watoaji wanavyojenga mtandao ambao unawawezesha kujuana na watu wapya na wanaokuwa msaada kwao baadaye.

Tutaangalia jinsi watoaji wanavyoshirikiana na wengine na kuwa na uzalishaji mkubwa kwenye kazi zao.

Kwa upande wa tathmini, tutaona jinsi watoaji wanavyowathamini wengine na kuwasaidia kupiga hatua zaidi, kitu kinachokuwa na manufaa kwao pia.

Na kwenye ushawishi, watoaji wamekuwa na mbinu inayowafanya wengine kukubaliana nao bila ya kutumia nguvu kubwa.

Tutajifunza misingi hiyo minne kupitia mifano ya waliofanikiwa sana na tafiti mbalimbali na kuondoka na hatua za kuchukua ili kuweza kuwa watoaji wanaonufaisha wengine na kunufaika wenyewe pia.

Sehemu ya pili ya kitabu tunakwenda kuangalia gharama au hasara ya utoaji. Kama ambavyo mpaka sasa utakuwa na wasiwasi, kwamba kwa kutoa sana, wengine watajinufaisha kupitia wewe. Hilo ni kweli kabisa, lakini watoaji wenye mafanikio wanajua jinsi ya kujikinga na hilo.

Hivyo kwenye sehemu hiyo tutaona jinsi ya kuzuia kutumiwa na wengine, kuepuka kuchoshwa na utoaji  na kulinda muda na thamani yako kitu ambacho kinaonekana ni kigumu unapokuwa mtoaji.

Hapa tutaona mifano mbalimbali ya watu walioweza kuvuka vikwazo hivyo vya utoaji na jinsi walivyonufaika zaidi.

Mpaka unafika mwisho wa kitabu, utakuwa umejifunza jinsi utoaji ulivyo na manufaa kwenye mafanikio na kujua tahadhari za kuchukua ili utoaji usiwe hasara kwako.

Mwisho utajifunza hatua za kuchukua ili kuweza kuwa mtoaji na kufanikiwa zaidi. Kitu kikubwa utakachojifunza ni kwamba kama utafanya haya unayojifunza ili ufanikiwe, unaweza usifanikiwe. Lakini kama utayafanya kama sehemu ya maisha yako, mafanikio yatakuja kwako.

Karibu upate uchambuzi kamili wa kitabu hiki na uweze kujua hatua sahihi za kuchukua ili kufa ikiwa zaidi kwenye maisha yako. Uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha GIVE AND TAKE unapatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kuusoma jiunge na channel hiyo kwa kufungua www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail  

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania