Hadithi za mafanikio zimekuwa kikwazo cha mafanikio kwa walio wengi.
Na wengi wanaokwamishwa na hadithi hizo ni wale ambao hawajajua nini hasa wanachotaka kwenye maisha yao.
Hivyo wakisoma hadithi moja ya mtu aliyefanikiwa kwenye kulima mpunga, wanapanga kwenda kulima mpunga.
Kesho wakisoma hadithi ya mtu mwingine aliyefanikiwa kwenye kufuga kuku, wanapanga kwenda kufuga kuku.
Kadhalika hata kwenye tabia za wale waliofanikiwa, leo mtu anasoma waliofanikiwa wanaamka mapema, anapanga kuanza kuamka mapema, siku nyingine anasoma waliofanikiwa wanachelewa kulala, anapanga kuchelewa kulala.
Kwa namna hii, wengi wamekuwa wanahangaika na hadithi za mafanikio na haziwasaidii chochote, wanahangaika na mengi ila mwisho wa siku wanajikuta wamerudi pale walipoanzia.
Kitu muhimu sana unachopaswa kujua ni kwamba hadithi za mafanikio hazitakupa kusudi, hazitakuambia nini unapaswa kufanya. Kama umesoma hadithi hizo kwa muda, utagundua watu wanafanikiwa kwenye kila jambo.
Hivyo lazima kwanza wewe mwenyewe ujue kusudi la maisha yako ni lipi, ujue nini unachotaka kufikia kwenye maisha yako, nini hasa unachotaka, ndoto zako ni zipi. Hilo lazima lianzie ndani yako mwenyewe.
Baada ya kujua unachotaka, hadithi za mafanikio zinapaswa kukupa hamasa ya kuchukua hatua kufika kule unakotaka kufika. Lakini siyo kwa kuiga kila walichofanya waliofanikiwa, bali kujenga mtazamo ambao watu hao walikuwa nao.
Usiigie kila walichofanya, bali iga mtazamo ambao wamekuwa nao na ukawawezesha kufanikiwa. Ona nidhamu ya kazi waliyonayo, jinsi wanavyojituma, jinsi wanavyokabiliana na kushindwa na hata namna wanavyoyapokea mafanikio. Hayo ndiyo ya msingi na yenye tija kwako kujifunza.
Kuiga na kufanya kile ambacho waliofanikiwa walifanya au wanafanya ni njia ya uhakika ya kushindwa, kwa sababu hata wao wenyewe, ingekuwa wanaanza tena upya leo, na wakafanya kila walichofanya, hawatapata mafanikio waliyopata.
Unachohitaji sana kwenye hadithi za waliofanikiwa siyo walichofanya, bali tabia na mitazamo ambayo wamekuwa nayo. Kwani ukijifunza hivyo na kufanyia kazi, utaweza kufanikiwa kwenye chochote unachofanya.
Muhimu kabisa ni usijaribu kuwa mtu mwingine yeyote, kuwa wewe. Kwenye hadithi za mafanikio utakazojifunza, utakutana na vitu ambavyo haviendani na wewe, mfano utakutana na watu ambao wanachelewa kulala, wakati wewe ukiwahi kuamka ndiyo unakuwa vizuri. Au unakutana na wanaowahi kuamka wakati wewe ukichelewa kulala ndiyo unafanya mambo mazuri.
Mwisho wa siku kuwa wewe, ila kuwa wewe ambaye ni bora zaidi na hapo utaweza kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,