Rafiki yangu mpendwa,
Ipo kauli inayosema haijalishi unajua nini, bali unamjua nani.
Nyingine inasema ukubwa wa utajiri wako (networth) unategemea ukubwa wa mtandao wako (network).

Kauli hizo mbili zinaonyesha umuhimu wa mtandao wa watu unaowajua na wanaokujua ili uweze kufanikiwa kwenye kile unachofanya, iwe ni kazi au biashara.

Chochote unachotaka, kipo kwa watu wengine.
Popote unapotaka kufika, kuna wengine unahitaji msaada wao.
Hivyo ni muhimu sana ujenge na kuimarisha mtandao wako ili uweze kupata mafanikio makubwa.

Tatizo kubwa la wengi kwenye kujenga mtandao huu wa mafanikio, ni kuamini kwenye njia moja tu ambayo imezoeleka.
Njia hiyo ni kukutana na watu kwenye maeneo ya starehe, hasa kwenye baa.

Utawasikia watu wakisema kabisa kwamba madili yapo baa. Kwamba wasipoenda baa hawawezi kupata madili mazuri.

Ni kweli mtu unaweza kupata madili baa, lakini muda unaotumia huko na vilevi unavyotumia vinakuwa na madhara kwako kuliko hata hayo madili unayopata.

Kukaa baa mpaka usiku wa manane huku ukitoka ukiwa umelewa siyo njia sahihi ya kujenga mafanikio yako.
Unapoteza muda  wingi na unauchosha mwili wako pamoja na kudhorotesha afya yako.

Mafanikio makubwa yanahitaji sana matumizi mazuri ya muda wako na mwili wako kuwa na nguvu ya kuweza kupambana. Kutegemea kwenda baa ili kujenga mtandao wako, inakwenda kinyume na hayo na hilo linakuwa kikwazo kwa mafanikio makubwa.

Hapa tutajifunza njia 10 za kujenga mtandao wako wa mafanikio bila kwenda baa.

Kabla ya kuingia kwenye njia hizo 10, kwanza kabisa lazima ujue ni watu gani muhimu unaowalenga.
Usihangaike tu na kila mtu, bali wajue wale wenye mamlaka na wafanya maamuzi ambao unawahitaji sana ili mambo yako yaende.

Ukishawajua hao muhimu, unaweza kutumia njia mbalimbali katika hizi kumi ili kujenga mahusiano mazuri na yakakuwezesha kupata unachotaka.

Kingine muhimu zaidi kwenye kujenga mtandao ni toa kabla hujaomba. Usimtafute mtu wakati una shida tu, hatakupa kipaumbele. Anza kumpa mtu kabla hata hujawa na uhitaji kwake na siku ukiwa na uhitaji atakuwa tayari kukupa kwa sababu kuna deni umejenga kwake kwa yale uliyompa.

Baada ya hayo muhimu, sasa ni njia 10 mbadala za kujenga mtandao wako ukiachana na baa.

1. Siku ya kuzaliwa.
Kila mtu ana siku yake ya kuzaliwa.
Jua tarehe za siku za kuzaliwa za wale unaotaka kujenga nao mahusiano mazuri na siku hiyo inapofika wasiliana nao kuwatakia heri na kuwapa zawadi mbalimbali.
Unaweza kuona ni kitu kidogo, lakini kina nguvu kubwa, mtu atakuthamini sana kwa kuithamini siku yake ya kuzaliwa.

2. Sherehe.
Watu huwa wanakuwa na sherehe mbalimbali na kwa taratibu zetu wengi huomba michango ili kukamilisha sherehe zao.
Jua sherehe za wale unaowalenga na changia kwenye sherehe zao.
Hilo litawafanya waone unawathamini na baadaye kuwa tayari kukupa kile unachohitaji kwao.

3. Misiba.
Watu huwa wanapata misiba ya watu wao wa karibu. Katika kipindi cha misiba watu huhitaji faraja na misaada mingine.
Jua pale unaowalenga wanapokuwa na misiba na uwe karibu nao, uwape faraja na kusaidia yale unayoweza.
Hilo litamfanya mtu awe na deni kwako unaloweza kulitumia kupata vitu vingine zaidi.

4. Dini.
Kama unayemlenga mpo kwenye dini au dhehebu moja, ni rahisi kujenga naye ukaribu zaidi.
Kwanza ni kupitia kushiriki ibada, ni rahisi kuonana na kusalimiana baada ya ibada.
Pili ni kamati mbalimbali zinazokuwepo ambapo unayemlenga anaweza kuwa kwenye moja ya kamati hizo, ukitafuta njia ya kuwa kwenye kamati hizo pia unapata fursa ya kuwa karibu na mkashirikiana.

5. Siasa.
Kupitia siasa pia unaweza kujenga mtandao wako.
Kwa kujua shughuli za kisiasa ambazo unayemlenga anashiriki na kuona jinsi unavyoweza kumsaidia.
Kama anagombea basi changia fedha kwenye kampeni zake.
Kaka ana harambee basi toa mchango wako.
Kwa kuwa sehemu ya harakati zake za kisiasa, unamjengea deni kwako.

6. Changamoto.
Kila mtu huwa ana changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo kwenye maisha yake.
Hata unayemlenga pia ana changamoto zake.
Ni wajibu wako kujua changamoto anazokabiliana nazo na kuona zipi unaweza kumsaidia kutatua kisha kufanya hivyo.
Msaidie kutatua changamoto bila kumwomba chochote, na siku ukiwa na uhitaji kwake atakupa kipaumbele.

7. Zawadi.
Unaweza kutafuta sababu yoyote ile ya kumpa zawadi mtu unayetaka kujenga naye mahusiano.
Landa amepanda cheo au amepata nafasi fulani nzuri, mpe zawadi.
Zawadi siyo lazima iwe kubwa sana, ni kitendo cha kutambua nafasi yake ndiyo chenye nguvu.

8. Mtandao.
Unaweza kujenga mtandao wako na mtu kwa kumsaidia kujenga mtandao wake. Angalia ni watu gani ambao unawajua na wanaweza kuwa msaada kwa yule unayemlenga.
Kisha wakutanishe pamoja ili waweze kushirikiana. Kama watakuwa sahihi kwa kila mmoja, watakuthamini sana wewe uliyewakutanisha.

9. Makongamano.
Makongamano mbalimbali kama semina, mikutano na maonyesho ni sehemu ya kukutana na watu muhimi na unaowahitaji zaidi.
Yajue makongamano muhimu ambayo wale unaowalenga wanahudhuria na wewe uhudhurie pia.
Tumia nafasi hiyo kukutana na wale muhimu na kuwapa kitu kitakachowafanya wakukumbuke na kukutafuta au ukiwatafuta wasiwe wamekusahau.

10. Vyama.
Kuna vyama mbalimbali ambavyo watu huwa wanachama. Hapa ni nje ya vyama vya siasa. Vinaweza kuwa vyama vya kitaaluma au vyama vya kijamii.
Jua vyama ambavyo unaowalenga wapo na kisha tafuta njia ya wewe kuwa mwanachama pia au kama haiwezekani tafuta njia ya kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za vyama hivyo.
Hilo litaleta ukaribu na wale unaowalenga.

Njia hizi, na nyingine ambazo umezifikiria baada ya kusoma hapa, zinaweza kukusaidia kujenga mtandao imara na utakaokusaidia kufanikiwa.

Tahadhari; njia hizi zina nguvu kubwa na unaweza kuzitumia kuwahadaa wengine. Lakini epuka sana hilo, ukiwahadaa watu utavunja kabisa uaminifu wako.
Tumia njia hizi kwa nia njema, kuwa mwaminifubna wasaidie kweli wengine.
Usitoe tu kwa sababu unategemea kupata, bali toa kuongeza thamani kwa mtu mwingine.

Kadiri unavyochukua hatua hizi kwa msimamo na kwa muda mrefu, ndivyo unavyojenga na kuimarisha mtandao wako.
Nikitakie kila la kheri katika kujenga mtandao bora kwa mafanikio yako.

Rafiki yako anayekupenda sana,
Muuza Matumaini Kocha Dr Makirita Amani,
www.somavitabu.co.tz

Pata vitabu hivi kwa kuwasiliana na 0752 977 170