Seth Godin ni mmoja wa watu bora wa masoko hapa duniani. Msingi wake mkuu wa masoko umebebwa kwenye moja ya vitabu vyake ambacho kimekuwa maarufu sana, alikiita kitabu hicho Purple Cow, yaani ng’ombe wa zambarau.
Anasema tumezoea kuwaona ng’ombe weusi, weupe na kahawia, hivyo huwezi kumkuta mtu anashangaa ona yule ng’ombe mweupe, ni kawaida, kila mtu anajua ng’ombe wanakuwa na rangi hizo.
Lakini siku ukikutana na ng’ombe wa rangi ya zambarau, utasimama na kushangaa, kwa sababu hujawahi kumwona ng’ombe wa aina hiyo.
Anachotufundisha Seth ni hiki, sokoni kuna bidhaa na huduma nyingi zinazofanana, kwenda na bidhaa ya aina hiyo sokoni hakutakupa manufaa, maana watu wameshazoea. Njia pekee ni kwenda na bidhaa au huduma ya tofauti, ambayo haijazoeleza, ambayo watu hawajawahi kuiona, na hapo watu watashangaa, watu watakuja kuijaribu na utaweza kuliteka soko.
Cha kusikitisha ni kwamba watu wengi wamelielewa somo la Seth, lakini utekelezaji wake umekuwa tofauti. Badala ya kuja na ng’ombe wa zambarau, wameamua kuja na mbwa anayetembea kwa miguu miwili.
Dhana ya mbwa anayetembea kwa miguu miwili ilielezewa na Samuel Johnsona ambaye amewahi kusema ukimuona mbwa anatembea kwa miguu miwili, hutaanga kama anatembea vizuri, bali utashangazwa na kuweza kwake kutembea hivyo.
Hatutegemei mbwa atembee kwa miguu miwili, hivyo tunapokutana na mbwa anayefanya hivyo, hatutaangalia kama anatembea vizuri, bali tutashangawa na hilo.
Hivi ndivyo wengi wanavyofanyia kazi dhana ya kujitofautisha, badala ya kujitofautisha kwa namna ambayo italeta thamani zaidi na hivyo kuwavutia watu sahihi, wanajitofautisha kwa namna ambayo itawashangaza wengi zaidi na kuleta umaarufu.
Hii wanaiita kiki na lawama zote ziende kwenye mitandao ya kijamii, kwani sasa kila mtu ana nafasi ya kufanya ujinga wowote anaoweza, ili tu awe maarufu, azungumziwe na wengi na kujulikana zaidi. Lakini aina hii ya utofauti imekuwa haidumu, kwa sababu wengi wapo tayari kufanya mambo ya kijinga zaidi na watu unaokuwa umewavutia siyo sahihi.
Kila mbinu ya kujitofautisha unayofanyia kazi jiulize kama ni ng’ombe wa zambarau au mbwa anayetembea kwa miguu miwili.
Ng’ombe wa zambarau anawavutia watu sahihi kwako, anaweza asikufanye maarufu lakini atakupa matokeo sahihi. Mbwa anayetembea kwa miguu miwili anavutia watu wasio sahihi kwako, atakufanya kuwa maarufu lakini hatakupa matokeo sahihi.
Kuwa makini, urahisi wa mitandao ya kijamii na wengine wanaofanya hivyo watakushawishi uone ni kawaida, lakini wewe fikiria miaka mingi ijayo, jenga jina na sifa itakayoheshimika kwa muda mrefu na siyo kukimbizana na umaarufu wa muda mfupi utakaokuwa kikwazo kwako kwa muda mrefu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,