Kwa kila jambo unalopanga kufanya, kuna hatari ya kupata matokeo mabaya na hivyo kushindwa. Kila kitu kina hatari hiyo, hata uwe na uhakika kiasi gani.

Hatari hiyo huwa inazalisha hofu ndani yetu, lakini kiwango cha hofu tunayokuwa nayo, huwa hakilingani na kiwango cha hatari.

Hofu tunayokuwa nayo hua inakua kadiri tunavyoipa nafasi, kadiri tunavyofikiria hatari iliyopo, ndivyo tunavyoona uwezekano mkubwa wa kutokea na hofu kuzidi kuwa kubwa.

Iwapo hutaifikiria sana hofu unayokuwa nayo, inakosa nguvu na kupotea yenyewe na hapo unabaki na nafasi ya kuchukua hatua sahihi.

Hofu zinawatisha na kuwakwamisha watu siyo kwa sababu ya ukubwa wake, bali kwa namna ambavyo watu wanazikuza, kufikiria kile unachohofia kwa muda mrefu kinaifanya hofu kuwa kubwa zaidi.

Hii ni kusema kwamba hofu haina nguvu yoyote, bali ile ambayo unaipa wewe. Usipoipa hofu nafasi, haipati nguvu ya kukutisha sana.

Hili linakupa machaguo mawili,

Kwa kila unalopanga kufanya, unaweza kuchagua kuikuza hofu uliyonayo kwa hatari inayokukabili, na hapo hofu ikawa kubwa na kupelekea kukuzuia usichukue hatua kabisa.

Au unaweza kuchagua kuchukua hatua, kwa kupeleka mawazo na nguvu zako kwenye kile unachotaka kufanya na hapo hofu inakosa nafasi na kupotea kabisa.

Huwezi kufanya yote mawili kwa pamoja, lazima uchague moja, kuikuza hofu au kuchukua hatua. Kwa kila unalopanga, chagua kwa usahihi, usije kulalamika baadaye kwamba hofu inakuwa kikwazo kwako, wakati wewe mwenyewe ndiye unayeipa nafasi ya kukua.

Tambua hofu inakuonesha hatari iko wapi, ukishajua hatari hiyo chukua tahadhari sahihi, lakini usiendelee kuweka mawazo yako kwenye hofu hiyo, badala yake peleka mawazo na nguvu kwenye hatua unazopaswa kuchukua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha