Kila kitu chenye thamani kwenye maisha, kina gharama, mafanikio yana gharama yake kubwa sana na ndiyo maana katika kila watu 100, ni mmoja pekee ambaye anakuwa na mafanikio makubwa.
Moja ya gharama kubwa ambayo mtu unapaswa kulipa kwenye mafanikio, ni kusimama kwenye ukweli. Kinachofanya mmoja kati ya 100 ndiyo afanikiwe, ni kwa sababu watu wote 100 wanakuwa wanaamini kitu kimoja, lakini mmoja anakataa kuamini tu kirahisi.
Anachagua kuutafuta ukweli, lakini wale 99 wanampinga kwamba anachotafuta siyo sahihi, bora aendelee kuwa nao. Mara kwa mara kuna wanaojaribu hivyo, lakini nguvu ya wale 99 inawarudisha nyuma. Ni mpaka pale anapotokea mmoja ambaye anaendelea kusimama licha ya kupingwa na wengine 99. Anaendelea kwenda licha ya kuanguka mara nyingi na kuambiwa tulikuambia.
Na baadaye, anakuja kupata kile ambacho 99 hawapati na anashangiliwa kwa mafanikio yake.
Kinachowaponza na kuwakatisha tamaa wengi wanaoianza safari ya mafanikio ni kutokuelewa pale mwanzoni wanapopingwa na kila mtu, pale ambapo hawaeleweki na wengine. Kwa kuwa wanawaangalia waliofanikiwa sasa ambao wanasifiwa, wanaona huenda wanachofanya wao siyo sahihi, kwa nini hawasifiwi kama waliofanikiwa.
Unachopaswa kujua ni kwamba, hawa wanaosifiwa leo kwa mafanikio yao, kabla hawajafanikiwa walikuwa wanapingwa na kudharauliwa. Lakini wao hawakusikiliza, walisimamia kile walichoamini na mwisho wakaweza kupata mafanikio na wale waliokuwa wanawadharau na kuwapiga, wakageuka kuwa wanaowasifia.
Hivyo kitu kimoja cha kujua na kusimamia ili ufanikiwe ni ukweli, hasa ukweli kuhusu wewe. Lazima ujijue wewe mwenyewe na uweze kuishi kama wewe, bila ya kujali wengine wanaishije.
Utakapochagua kuyaishi maisha yako, kuna gharama nyingi utalipa, kuna ambao watakunyima fursa nzuri, wapo watakaokukwamisha makusudi na wengine watakulazimisha ubadilike ili wakupe unachotaka.
Utakapobadili msimamo na kuanza kuishi kuwafurahisha wengine, hapo ndipo utakapokuwa umeagana na mafanikio yako na kukubali kuwa kawaida.
Lazima ujue wazi kwamba kwa maisha yoyote utakayochagua kuishi, kwa chochote utakachoamua kufanya kwa tofauti, utakutana na upinzani mkali, kutoka kwa wale ambao wamekuwa wanafanya kwa mazoea. Watakuambia hiyo siyo njia sahihi ya kufanya, watakuambia umekiuka misingi au miiko na mengine mengi.
Unapaswa kujua kila aliyeleta mabadiliko kwenye eneo lolote lile, alikubali kwenda kinyume na wengi na alikutana na upinzani mkali kutoka kwa wengine. Lakini hakukubali kurudi nyuma, na hilo lilimpa mafanikio, huku wale waliokuwa wakimpinga wakiwa wa kwanza kumsifia baada ya kufanikiwa.
Una majaribu mengi na makubwa mbele yako, kuyavuka inakutaka ujitoe sana, usimamie ukweli, ulipe gharama. Mara zote jua utakuwa mmoja unayekabiliana na 99 wanaotaka uwe kama wao. Jiandae na pambana kikamilifu. Mafanikio siyo rahisi, ndiyo maana wengi hawayapati.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
asante sana Kocha
Nimejifunza ni bora kupokea leo ukweli na maumivu yake,kuliko kupokea uogo kesho yangu haitakuwa bora sana
LikeLike
Vizuri Mary.
LikeLike
asante kocha
LikeLike
Karibu Alex.
LikeLike