Hatua unazopiga na matokeo unayopata, vinategemea sana aina ya watu waliokuzunguka.

Watu hao wanagawanyika kwenye makundi mawili na ndani ya kila kundi wanagawanyika mara mbili.

Kundi la kwanza ni wale wanaokutia moyo na kukushauri upige hatua zaidi. Hawa wanakubaliana na kile unachofanya na wanakupa sababu ya kuendelea. Ni rahisi kuwapenda na kuwasikiliza watu hawa, lakini kuwa makini.

Kuna watia moyo wa aina mbili, kwanza ni wale ambao wanataka kweli upige hatua na wapo tayari kukusaidia na kukusukuma zaidi ufanikiwe. Pili kuna watua moyo ambao wanaogopa kukuambia ukweli, ndani yao wanajua kabisa utashindwa au utakutana na ugumu, lakini hawataki kukukatisha tamaa, hivyo wanakutia tu moyo, ukishindwe ushindwe mwenyewe wasije kuonekana wao ndiyo waliokukatisha tamaa.

Unapaswa kuwajua watia moyo ambao wanataka kweli ufanikiwe, ambao hawaogopi kukuambia ukweli ambao utakuumiza. Lengo lao ni kukuona wewe unapiga hatua. Waepuke watia moyo ambao wanaonekana kukubaliana na wewe kwa kila kitu, hata ambacho wewe mwenyewe unajua siyo sahihi.

Kundi la pili ni wale wanaokukosoa, wale ambao wanatafuta makosa kwenye kile unachofanya. Watu hawa wanaonesha wazi wazi kwamba kuna mambo unayofanya na hawakubaliani nayo au siyo sahihi kwa mtazamo wao. Ni rahisi kuwachukia watu hawa, na kuona hawakutakii mema, lakini siyo wote wana nia mbaya. Kwani wakosoaji wamegawanyika makundi mawili pia.

Kuna wakosoaji ambao lengo lao ni kukushusha wewe, hawa hawataki kuona ukipiga hatua hivyo watatafuta hata vitu visivyo muhimu na kuviibua, lengo ni kukuvuruga usipige hatua. Halafu kuna wakosoaji ambao wana lengo la kukusaidia upige hatua, wanaokuonesha yalipo madhaifu yako ili uweze kuyaimarisha zaidi.

Unapaswa kuwajua wakosoaji wenye lengo la kukusaidia upige hatua na kisha kuwasikiliza, maana hao wanaonesha madhaifu yako. Wakosoaji wa kuachana nao ni wale wanaotaka kukuangusha ili wao wawe juu.

Utawajua watia moyo na wakosoaji sahihi kwa namna wanavyobeba kile unachofanya. Wasio sahihi watajua juu juu tu, hawatajisumbua kujua unachofanya kwa kina, ila wenye nia njema, watakazana kujua kwa kina na mchango watakaotoa utakuwa wenye manufaa kweli.

Unasikiliza watu wa aina gani? Hili ni swali la kujiuliza na kujitathmini kwa wale wanaokuzunguka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha