Kama umeingia kwenye maji ya kina kirefu na uko kwenye hatari ya kuzama huku ukiwa huna kifaa cha kujiokoa, akitokea mtu anayeuza vifaa vya kujiokoa kwenye maji hutauliza mara mbili. Utakachokifanya ni kununua kifaa hicho ili uokoe uhai wako kwanza, maana hicho ndiyo muhimu zaidi kwako kwa wakati huo.
Mtu mwenye kifaa cha kuokoa maisha, hahitaji kuwa na tangazo la kushawishi watu kununua kifaa anachouza, anachohitaji ni kumfikia mtu aliye kwenye hatari ya kuzama na mtu huyo atanua bila hata kusubiri kushawishiwa.
Kuna kitu kikubwa cha kujifunza kwenye hili, kwa kazi au biashara unayofanya, kama unateseka kupata watu wa kuithamini au wateja wa kununua unachouza ni kwa sababu hujawajua watu sahihi au kama umewajua basi hujaweza kuwafikia wakiwa kwenye hali za hatari inayowasukuma kutaka unachotoa.
Ni wajibu wako kujua kile unachofanya au kuuza kinatatua hatari ipi kubwa kwa yule unayemlenga, kisha jua ni wakati gani mtu huyo anakuwa kwenye hatari inayoweza kumpoteza kabisa, na hapo jitokeze ukiwa na suluhisho lako, ambalo ndiyo kitu pekee kinachoweza kumsaidia. Hutahitaji kupiga kelele, ataona alichotaka na atakichukua.
Tunatumia nguvu nyingi na kuhangaika na mengi yasiyo sahihi, kama tukielekeza hayo kwenye machache yaliyo sahihi, matokeo tutakayoyapata yatakuwa makubwa.
Chochote unachofanya, kijue kwa undani kiasi hicho, kwa kuweza kujua hatari ambayo mtu anapitia na unachofanya ndiyo ukombozi wake, kisha kuwa pale hatari inapotokea.
Tahadhari; katika kipindi ambacho mtu yupo kwenye hatari, anaweza kukubaliana na chochote na hapo unaweza kufanya kitu kitakachomuumiza. Epuka sana ushawishi wa kufanya hivyo, fanya kile kilicho sahihi, ambacho hata kama ingekuwa wewe unafanyiwa, basi ungefurahia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana kocha .
LikeLike
asante sana kocha
LikeLike