Zama tuishizo sasa ni zama ambazo maisha yetu kwa asilimia kubwa tunayatumia mitandaoni. Iwe ni katika kuhitaji huduma au ununuzi wa bidhaa au mawasiliano na watu yote yanafanyika kwa njia ya mtandao. Hili limefanya kuwa taarifa au habari zinazotokea eneo lingine la Dunia kuwa rahisi kutufikia kwa njia ya mtandao kwa watumizi wa vifaa vyote vya mawasiliano. Iwe ni simu au tarakilishi [kompyuta]. Licha fursa hii ya mtandao kuwepo na kuunganisha watu kuna changamoto zake nyingi ambazo mwandishi Ashesh ameziita gharama tano za kuishi mtandaoni.

Mosi ni juu ya ushawishi mkubwa. Unaweza kusema ngoja uingie utafute taarifa ulizokuwa unazihitaji unaishia kutumia masaa au pengine siku nzima ukiwa umependezwa na tovuti zingine. Watu wengi wanaweza kusema ngoja niingie niangalie katika makundi ya mitandao ya kijamii kuna kitu gani. Wakija kupata ufahamu masaa yameshapita na wamechoka akili kwa kuingiza taarifa ambazo hawakutarajia kama wangeruhusu zipite katika fikra zao.

Urahisi wa kupata kila kitu kupatikana mtandaoni kumefanya hata watu wajikute wanaishia kushawishiwa na kuangalia picha chafu ambazo mwisho wa siku zinafanya watu wawe watumwa kuendelea kuangalia bila kuziacha. Uwepo wa matangazo mbalimbali ya kuamsha tamaa za mwili nayo yamefanya watu washindwe kujizuia kuacha kuyafuatilia hadi kuweza kupata huduma zake. Kushinda hili inahitajika nidhamu kubwa na nguvu kubwa ya kujizuia lasivyo mitandao itakuwa sawa na utando wa buibui wenye kunasa wadudu wapitao. Kujizuia kutumia muda zaidi ya ule ulojipangia, kujizuia kuangalia picha chafu na michezo isofaa kunaweza kusaidia kushinda mtego huu ambao umewanasa watu wengi.

Pili ni taarifa kuwa nyingi kuliko muda wa kuzifuatilia na hivyo kufanya uchaguzi wa taarifa ipi ni sahihi na ipi ya kuacha hubakia changamoto. Taarifa zinazosambaa na kushirikishwa kupitia mitandao ya kijamii ni nyingi na kila siku huongezeka. Hivyo pamekuwa na mafuriko ya taarifa na maarifa. Haijawa taabu kama zamani kuwa wapi ungepata taarifa. Sasa kuna vyanzo vingi vya taarifa mtandaoni kuanzia redio za mtandaoni, magazeti ya mtandaoni, majukwaa ya mtandaoni. Vyanzo vyote hivi husambaza taarifa kwa watu.

Taarifa hizi zimesababisha watu wawe na uvivu na uzembe au kuachwa njia panda washike taarifa ipi na kuacha taarifa zipi. Baadala ya kusaidia watu wawe na taarifa ziwasaidie lakini zimefanya watu washindwe kabisa kufanya maamuzi ya kuzifanyia kazi sababu ya wingi wake na wanashindwa kutofautisha zipi ni taarifa sahihi na zipi si sahihi. Hili imekuwa changamoto inayoonekana hata kwenye makundi ya kijamii kama “Whatsapp” kuwepo kwa taarifa au maarifa mengi yanayoendelea kushirikishwa. Inahitaji kuwa makini na kuchagua maarifa machache na vyanzo unavyoviamini kuwa kama chanzo chako cha maarifa au taarifa kuepuka kutaka kupata taarifa toka kila chanzo.

Tatu ni mapendekezo na matangazo ya bidhaa ni mengi. Unapofungua mtandao wa kijamii au kutafuta taarifa kupitia mtandaoni unakutana na mapendekezo ya matangazo mengi ambayo kwa kutokuwa tayari kupata huduma zake unajikuta unafuatilia au kununua kabisa. Hili limekuwa linaleta usumbufu mkubwa unapokuwa mtandaoni. Machagulio na matangazo unapoangalia vitu iwe ni taarifa, picha mjongeo unakutana nayo yanakuja na kwa namna moja yanaharibu utulivu na kuingiza usumbufu usio na tija kwako.

Nne ni ulinganifu wa maisha kwa kile watu wanachoshirikisha kupitia mtandao wa kijamii. Kama viumbe wa jamii huwa ni asili kujilinganisha na wengine. Lakini kwa njia hii ya mtandao ulinganifu huwa si halisi wa watu kushirikisha maisha ambayo si halisi na kufanya wengine wajisikie vibaya wanapoangalia maisha yao.

Watu wengi wamejikuta wakiingia gharama ya maisha ya juu ambayo wanaishia kuyaweka mtandaoni na huku katika uhalisia wakiishia katika madeni makubwa. Kitendo hiki kimewaletea watu kuwa na maisha ya kuigiza na hofu pale ambapo maisha yao halisi yakiwekwa wazi. Kumbuka kuwa watu wanachoshirikisha mtandaoni ni sehemu ndogo ya maisha yao. Na isitoshe kinachoshirikishwa ni upande ulio bora tu unaofanya wengine waone kuwa maisha yao ndio yenye magumu na si watu wote. Ukiweza kugundua hili itakusaidia kujiboresha wewe mwenyewe katika uhalisia wako wa maisha na si kufanya kitu ili ufanye tu kuwaridhisha wengine.

Tano ni usiri mdogo sana mtandaoni. Ikumbukwe kuwa hakuna kinachosahaulika mtandaoni. Vingi huhifadhika na kutumika kama rejea hapo baadaye. Kila kinachofanyika mtandaoni huwa kimfumo hujirekodi na hii ndio inasaidia wengine kubuni bidhaa ambazo zinaendana na vitu gani watu hufuatilia kupitia njia ya mtandao.

Usiri ni hali ambayo kila mtu huipendelea. Ila watu wengi wamejisahau pale ambapo wanashirikisha maisha yao kupitia mtandao wasijue kidogo kidogo wanayaanika maisha yao kwa watu wengi. Licha kuwepo kwa makampuni yanayojitahidi kulinda usiri wa watumiaji wake katika kupata huduma au bidhaa wanazotaka au taarifa. Hitaji la mtumiaji wa mitandao kuwa makini na taarifa ambazo anakuwa anashirikisha kupitia mitandao ya kijamii.

Linda muda na nguvu zako ambazo ni mhimili katika kufikia malengo yako. Jiwekee nidhamu ambayo itakuwa na tija katika kutumia mtandao kwa kiasi na kwa faida. Ukiweza kudhibiti muda wako na nguvu kutopotelea kuzurura mtandaoni unaweza kufanya mambo makubwa na maisha yako.  

Mchambuzi,

Dkt.Raymond Nusura Mgeni

raymondpoet@yahoo.com

+255 676 559 211.