“Hurried work done in irritation attracts the unfavorable attention of others. Real work is always quiet, constant, and inconspicuous.” – Leo Tolstoy

Kazi isiyo sahihi, inayofanywa kwa haraka na kelele nyingi, huwa inawavutia wengi na kuonekana ni maarufu.
Lakini huwa siyo kazi sahihi na matokeo yake huleta uharibifu kwa wengi.

Kazi iliyo sahihi huwa inafanyika kwa ukimya, ni ya msimamo na isiyovutia wengi.
Matokeo ya kazi hiyo huwa makubwa na bora na kumwezesha kupiga hatua.

Kikwazo kikubwa cha wengi kufanikiwa kwenye kazi zao ni kutafuta umaarufu kupitia kazi hizo, badala ya kuweka kazi na kuzalisha matokeo ambayo ni bora.

Mitandao ya kijamii imekuwa sumu kubwa,
Badala ya mtu kuweka muda na umakini kwenye kazi yake, anatumia muda huo kujenga umaarufu kwenye mitandao ya kijamii, kuonekana anafanya kazi fulani.

Wasichojua wale wanaopiga kelele mitandaoni ili kupata umaarufu ni kwamba kila mtu anapiga kelele za aina hiyo akiamini zinampa umaarufu.
Njia sahihi ya kupata mafanikio makubwa, ambayo yatakuletea umaarufu pia ni kufanya kazi yako kwa namna ya kipekee.
Na ili uweze kufanya hivyo lazima ujichimbie kwa muda, lazima ufanye kazi yako kimya kimya kwa kufanya kilicho sahihi na kuzalisha matokeo.

Hata visirani watu wamekuwa wanavivuta kwa namna hii.
Mtu ameanza biashara ambayo bado hata hajaijengea misingi, anakimbilia kwenye mitandao ya kijamii kuonesha kila anachofanya.
Kinachotokea ni anashindwa na kujiona ana kisirani.
Ukweli ni kwamba, mtu anakuwa amekaribisha kisirani yeye mwenyewe.

Chagua kufanya kazi iliyo sahihi, ifanye kimya kimya na zalisha matokeo ambayo ni bora na ya kipekee kabisa.
Matokeo hayo yatajisemea yenyewe na kukuletea mengi.
Lakini kupoteza muda wako kwenye makelele au kama wanavyoita ‘kiki’ ukiamini yatakuletea umaarufu na mafanikio ni kujidanganya.
Kila mtu ndivyo anavyofikiria na kufanya.
Na kumbuka kitu kinachofanywa na kila mtu, huwa hakina thamani.

Usitafute umaarufu uchwara, tafuta mafanikio makubwa na hayo ukiyapata, yatakuja na umaarufu sahihi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kufanya yako na kuiacha dunia ifanye yake, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/09/24/2094

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.