Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu kinachoitwa SIDDHARTHA; An Indian Tale kilichoandikwa na Hermann Hesse.

Siddhartha ni riwaya iliyoandikwa na aliyekuwa mwandishi wa Ujerumani Hermann Hesse. Riwaya hii iliandikwa mwaka 1922 na inaelezea safari ya kiroho na kujitambua ya kijana aliyeitwa Siddhartha. Hii ilikuwa riwaya ya tisa ya mwandishi huyo na ambayo ilipokelewa vizuri na dunia baada ya kufika nchini Marekani mwaka 1951.

Neno Siddhartha linaundwa na maneno mawili kutoka kwenye lugha ya Sanskrit ya Kihindi. Maneno hayo ni siddha (aliyepata) + artha (alichokuwa anatafuta), hivyo kwa pamoja Siddhartha inamaanisha yule aliyepata maana ya maisha au aliyefikia malengo yake.

Riwaya kwa ufupi.

Siddhartha ni kijana aliyekulia kwenye familia ya jamii ya Brahman, familia yenye mafanikio makubwa kimali na iliyofikia ngazi za juu kiimani na kiroho. Siddhartha anapendwa na kila mtu na anategemewa kuja kuwa kiongozi wa kiroho, kwani tangu akiwa mtoto amekuwa akifanya ibada na tahajudi ambazo ni za viwango vya juu.

Lakini ndani yake kuna kitu hakiko sawa, licha ya mali zilizopo kwenye familia, licha ya kuwa juu kiroho, bado ndani yake hana furaha. Siddhartha anajaribu kutafakari wale wote wanaomzunguka, kuanzia baba yake na watu wengine na anaona wote hawana furaha, kwa sababu bado kuna kitu wanatafuta.

Siddhartha anaamua kuiacha familia yake na jamii yake na kujiunga na kikundi cha Samanas ambao ni watafutaji wa kiroho ambao wameamua kuchana na mambo ya dunia na kuishi porini. Govinda ambaye ni rafiki wa karibu wa Siddhartha anaungana naye na kwa miaka mitatu wanakaa na Samanas na kujifunza jinsi ya kuvumilia maumivu na njaa ili kuvuka ukomo wa mwili.

Pamoja na kujifunza mengi kutoka kwa Samanas bado Siddhartha hajaridhika, bado anaona kuna kitu kinakosekana ndani yake. Wanasikia kuhusu mafundisho ya Gotama Buddha na Siddhartha anaamua wakayasikilize pia. Wawili hao wanaenda kwenye mafundisho ya Buddha na mara baada ya kuyasikia, Govinda anachagua kujiunga na kuwa mfuasi, lakini Siddhartha anakataa kujiunga, akieleza kwamba kile anachokitafuta, hataweza kukipata kwa Buddha.

Siddhartha anaendelea na safari na kufika mji wa karibu ambapo anakutana na mwanamke mrembo anayeitwa Kamala. Mwanamke huyo hutumia urembo wake kuwashawishi wanaume kumpa kile anachotaka. Siddhartha anavutiwa naye na kumwomba mwanamke huyo awe mwalimu wake, amfundishe sanaa ya mapenzi. Kamala anampa sharti kwamba lazima awe na fedha, nguo nzuri na viatu ndiyo waweze kuwa pamoja.

Kwa hekima alizonazo, Siddhartha anapata kazi kwa mfanyabiashara mkubwa aitwaye Kamaswami na yeye na Kamala wanakuwa wapenzi. Siddhartha anapata mafanikio makubwa kwenye biashara anazofanya, anapata mali nyingi na kuishi maisha ya anasa. Anasahau mafunzo yote aliyekuwa ameyapata ya kujidhibiti na kuwa na nidhamu, anaanza kuwa mlevi na mcheza kamari.

Baada ya miaka, Siddhartha anaamka kama aliyetoka usingizini na kuona maisha ambayo amekuwa anayaishi siyo aliyotumia miaka mingi kuyatafuta. Anaamua kuondoka na kuacha kila kitu, kurudi kutafuta kile ambacho bado hajakipata.

Katika kutembea kwake, Siddhartha anakutana tena na Govinda, ambaye sasa ameshakuwa mtawa na mfuasi mkubwa wa Buddha. Siddhartha anaendelea kutembea na kufika kwenye mto, ambapo anakutana na mwendesha kivuko anayeitwa Vasudeva. Siddhartha anamuona Vasudeva kuwa mtu aliyetulia na anayeonekana kuwa ameshapata anachotafuta, hivyo anamuomba awe mwanafunzi wake, Vesudeva anakubali. Wawili hao wanaishi pamoja na Vesudeva anamfundisha Siddhartha jinsi ya kuusikiliza mto, ambao unajua kila kitu na una majibu ya chochote ambacho mtu amekwama. Kwa Vesudeva, mto ndiyo mwongozo wake mkuu wa kiroho.

Siddhartha anaishi na Vesudeva kwa miaka mingi, anakua zaidi kihekima kadiri muda unavyokwenda na kuweza kuusikiliza mto. Anakuja kukutana na mtoto wake ambaye alimwachia ujauzito Kamala na wanakaa kwa kipindi kifupi ila naye anaondoka kwenda kutafuta maisha yake.

Kupitia kuusikiliza mto na kwa mwongozo wa Vesudeva, Siddhartha anafanikiwa kufikia utambuzi wa juu (enlightenment) na Vesudeva anaondoka na kumuacha. Siddhartha anakutana tena na rafiki yake Govinda, wote wameshakuwa wazee lakini bado Govinda anahangaika kutafuta kile ambacho anaona hajakifikia. Siddhartha anamsaidia Govinda naye kufikia utambuzi wa juu.

Karibu kwenye uchambuzi.

Kitabu hiki kina sehemu mbili ila uchambuzi wetu utakuwa na sehemu tatu.

Kwenye sehemu ya kwanza ya uchambuzi tutaona safari ya Siddhartha kuondoka kwenye familia yake na kwenda kuishi na Samanas mpaka kukutana na Buddha. Hapa tunaona kiu ambayo Siddhartha anayo ya kufikia utulivu wa kiroho, ambao anaona hawezi kuufikia kwa kuendelea kubaki kwenye jamii yake. Lakini mwisho wa siku hafikii lengo lake kupitia kule alikoenda.

Kwenye sehemu ya pili ya uchambuzi tutaona maisha ya kidunia ya Siddhartha ambapo anapata mafanikio makubwa na kuishi kwa anasa na kusahau yote aliyojifunza. Tutaona mpaka pale anapokumbuka kurudi kwenye mafundisho sahihi.

Sehemu ya tatu ya uchambuzi tutayaona maisha ya Siddhartha baada ya kurudi kwenye mafunzo ya kiroho, akiishi na Vesudeva kama mwendesha kivuko na akijifunza na kufikia utambuzi wa juu wa kiroho kwa kuongozwa na mto. Pia tutaona anavyomsaidia rafiki yake naye afiki utambuzi wa juu.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hiki, ambapo tutajifunza mengi yatakayotusaidia kwenye safari yetu ya kiroho. Kubwa zaidi likiwa kujua maana ya maisha yako na ambayo unaweza kuipata popote ulipo bila hata kwenda kuitafuta mbali.

Kingine kikubwa ambacho hadithi ya Siddhartha inakwenda kutufundisha ni kwamba ukuaji wa kiroho hauwezi kufundishwa, bali unafikiwa kwa juhudi za mtu. Hata mwalimu au kiongozi awe mzuri kiasi gani, hawezi kumfundisha mtu mwingine jinsi ya kufikia ukuaji wa kiroho na utambuzi wa juu, anachoweza ni kumpa miongozo sahihi ya kufanyia kazi na kufikia yeye mwenyewe.

Siddhartha aliweza kuliona hilo kwa Buddha, pamoja na yeye mwenyewe kuwa amefikia utambuzi wa juu, mafunzo yake yasingewawezesha wanafunzi wake kufikia utambuzi huo. Alipokuja kukutana na mwendesha kivuko Vesudeva aliweza kupata mwongozo sahihi na yeye mwenyewe akafikia ukuaji wa kiroho na utambuzi wa juu.

Kupata uchambuzi kamili wa kitabu hiki cha SIDDHARTHA pamoja na vitabu vingine vizuri kwa mafanikio, karibu ujiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN CHANNEL.

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.