Muda ni changamoto kwa kila mtu, kila mtu hana muda na kila mtu anapoteza muda. Yaani ni sawa na kumkuta mtu anakulalamikia hana fedha, lakini wakati huo huo anachukua fedha na kuzitupa.
Kwenye fedha inaonekana haraka, lakini kwenye muda haionekani, kwa sababu muda huwa unatuponyoka.
Mtu anaweza kupambana apate muda zaidi kwenye maisha yake, anaupata kweli, lakini muda huo unapotea kwenye mambo yasiyo na manufaa.
Unaweza kumsikia mtu akijisifu kwamba kazi au biashara anayoifanya inampa muda mwingi wa kufanya ‘mambo yake’ lakini unapoangalia mambo hayo ni yapi, huyaoni.
Au mtu aliyekuwa anapoteza muda kwenye mitandao ya kijamii anaamua kuachana nayo, anapata muda zaidi, lakini hawezi kueleza huo muda alioukomboa kwenye mitandao ya kijamii umeenda wapi.
Muda una tabia ya kujaa kila unapopatikana. Kama ulikuwa unafanya kazi siku 7 na ukapambana upate siku moja ya kupumzika, kama hutailinda na kuipangilia vizuri siku hiyo, unakuja kukuta imeshajaa na huna tena muda.
Mtu anapokuwa na muda mwingi ambao haujapangiliwa kitu cha kufanyia, hujikuta anakaribisha mpaka mambo maovu kwenye maisha yao, ambayo yanazalisha changamoto zaidi.
Ili kuondokana na hali hii, pangilia kila muda wako. Usiwe na muda ambao upo tu, hakuna ulichojipangia kufanya.
Unapoianza siku yako, pangilia muda wa siku nzima, wakati gani utafanya nini. Pangilia mpaka muda ambao utapumzika kwenye siku yako na kisha fuata kile ulichopanga.
Ukianza siku kwa kujiambia unajua nini cha kufanyia kazi, utaimaliza siku ukiwa umechoka, huku kiwa huoni kipi kikubwa umefanya.
Linda muda wako kuliko kitu kingine chochote, kwa sababu ndiyo kitu chenye thamani zaidi kwako, ndiyo maisha yako. Usifurahie tu kupata muda zaidi, bali pangilia muda huo wa zaidi ulioupata kufanya mambo ambayo yataacha alama kwenye maisha yako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,