Ni watu wachache sana ambao huwa wanafanya makosa kwa kusudia. Wengi huwa wanaanza na nia njema kabisa, lakini matokeo yanakuja kuwa makosa makubwa na yenye madhara.
Mara nyingi tunapofanya maamuzi ya kufanya kitu, huwa tunaamini hatua tunazokwenda kuchukua zitarahisisha zaidi hali kuliko ilivyo sasa.
Mfano mtu anapochukua hatua ya kudanganya, ni kwa sababu anaona ukweli ni mzito au mchungu kwa hali iliyopo, hivyo kudanganya kutafanya mambo yawe rahisi.
Hata wale wanaoiba, mara nyingi huona hiyo ndiyo njia pekee wanayoweza kutumia kukabiliana na kile kilicho mbele yao.
Kila anayejikuta kwenye matatizo makubwa, mwanzo alianza kwa nia njema, lakini baada ya kufanya mara moja, alijikuta akiendelea kufanya kisha baadaye ikawa tabia inayopelekea kwenye matatizo.
Kwa kujua hili, tunapaswa kuwa makini na chochote tunachofanya, tusiangalie tu nia ya kufanya kitu hicho, badala yake tuangalie tabia itakayojengeka na kujiuliza iwapo tunataka kuishi na tabia hiyo.
Mfano unaona uko kwenye hali ambayo ukweli ni mchungu sana kueleza, ila unaweza kutumia uongo na ukavuka hilo bila ya madhara. Unaweza kushawishika kutumia uongo kwa hapo, lakini shida siyo uongo utakaotumia mara moja, bali tabia ya uongo itakayojengeka baada ya hapo. Hiyo ndiyo inayokuja kutengeneza matatizo makubwa na kukupoteza.
Kumbuka, ni vigumu kufanya kitu chochote kwa mara ya kwanza, lakini ukishafanya hata mara moja tu, ni rahisi kurudia tena kufanya.
Hivyo mara zote fanya kilicho sahihi, hata kama itakugharimu, wacha ikugharimu sasa kuliko kujenga tabia ambayo itakuja kukugharimu kwa kiasi kikubwa baadaye.
Nia njema isiwe kigezo cha wewe kufanya maamuzi ya hatua unazokwenda kuchukua, bali usahihi wa kitu, fanya kilicho sahihi mara zote, kwa sababu hicho pekee ndicho kitakachokuepusha na matatizo yasiyo ya lazima na yanayokwamisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,