Kinachowaangusha wengi kwenye hadithi za mafanikio ni hiki; kuangalia pale waliofanikiwa wapo sasa na kutaka kufika hapo,  bila kupitia mchakato wa kufika pale.

Yeyote unayemuona amefanikiwa leo, hakuamka na kujikuta kwenye mafanikio hayo, na wala hakupita njia ya mkato isiyohitaji kazi.

Alipitia kwenye mchakato mrefu ambao huwa haupewi uzito sana mtu akishafanikiwa.

Wewe usidanganyike na pale mtu alipo sasa, jua kuna mchakato ambao kila mtu lazima aupitie na wewe siyo maalumu sana kwamba hupaswi kuupitia.

Jipe muda wa kuyafikia mafanikio, jipe muda wa kupata matokeo unayotazamia kupata. Usiwe mtu wa kukata tamaa mapema kwa sababu matokeo unayotazamia hayaji kwa muda uliotegemea yaje. Mambo mazuri huwa yanachukua muda kujijenga.

Safari ya mafanikio ni mchakato, kwako binafsi na kwenye kile unachofanya. Kuna mabadiliko ambayo lazima uyapitie ili mafanikio yaweze kuja na yadumu na wewe. Kuna matokeo lazima uyazalishe ili yaweze kuvutia mafanikio kwako.

Kuna watu wataibua tamaa zako kwenye safari yako ya mafanikio, watakuja kwako na fursa wanazoziita mpya na za moto, wakikuambia ni njia za mkato za kufanikiwa na ambazo hazihitaji wewe kuweka kazi.

Unaweza ukashawishika na kujiambia utajaribu tu kwa muda, lakini jua hilo ni kama sumu, ukali wa sumu haupimwi kwa kuonja. Utakapokubali tu kujaribu njia hizo za mkato, ni sawa na umekunywa sumu, unakuwa umejipoteza kabisa.

Chochote unachofanya, kinaathiri kile unachoamini. Unapojaribu njia za mkato, unabadili kabisa imani yako na kuacha kuamini misingi sahihi. Ndiyo maana watu wakishaanza kujaribu njia za mkato, huwa hawaachi, watahangaika na njia nyingi, huku wakipoteza muda lakini hawataona hilo.

Simama kwenye msingi sahihi, chukua hatua unazopaswa kuchukua na kuwa tayari kwa mchakato sahihi wa kuyafikia mafanikio yako makubwa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha