Sehemu kubwa ya matatizo yanayowasumbua wengi kwenye maisha siyo matatizo halisi, bali tatizo la msingi linakuwa ni fedha.

Kama una tatizo lolote linalokusumbua na unaweza kulitatua kwa fedha, basi jua huna tatizo, bali unachokosa ni fedha.

Kwa kujua hili, inakupunguzia mzigo wa mawazo na msongo ambao umekuwa unajipa kwa matatizo yanayokuzunguka. Mengi umekuwa unayaona kama matatizo makubwa na mwisho wa dunia, kumbe ukiwa na kiasi fulani cha fedha yanapotea kabisa.

Hii haimaanishi kwamba kila tatizo linaweza kutatuliwa na fedha, lakini sehemu kubwa kabisa ya matatizo yanayokusumbua, fedha inaweza kuyatatua au kupunguza makali yake.

Hivyo tafakari matatizo yote unayopitia sasa na kwa kila tatizo jiulize iwapo fedha inaweza kutatua, kama jibu ni ndiyo basi jiambie wazi kwamba huna tatizo kwenye eneo hilo, bali unachokosa ni fedha.

Unapojua unachokosa ni fedha, unaenda moja kwa moja kwenye tatizo hilo la msingi, kuhakikisha unapata fedha za kutosha kutatua tatizo hilo na mengine yanayoendana na hilo.

Usijipe msongo mara mbili, msongo wa fedha na matatizo ambayo fedha inaweza kutatua. Badala yake yaweke matatizo yote ambayo fedha inaweza kutatua kwenye tatizo moja ambalo ni fedha, kisha weka juhudi kwenye kukuza kipato chako zaidi.

Tahadhari, huwa ni tabia ya wanadamu pale kipato kinapokua basi hutengeneza matatizo mapya na kuyatatua kwa ongezeko lao la kipato. Jiepushe na hili, usiwe mtu wa kutengeneza matatizo kwa sababu fedha ya kuyatatua ipo, bali kuwa mtu wa kutengeneza fedha ili kuhakikisha hakuna tatizo linalotatuliwa na fedha linakusumbua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha