“Most people are proud, not of those things which arouse respect, but of those which are unnecessary, or even harmful: fame, power, and wealth.” – Leo Tolstoy

Watu wengi wamekuwa wanajivunia siyo kwa vitu ambavyo vinaleta heshima kwao, bali kwa vitu visivyo muhimu na wakati mwingine vyenye madhara.
Vitu vitatu vikuu ambavyo wengi wamekuwa wanajivunia navyo na havina manufaa makubwa kwao ni umaarufu, madaraka na utajiri.
Na siku hizi watu wamekuwa wanajivunia vitu vya kijinga kabisa kama idadi ya wafuasi mtandaoni, idadi ya ‘likes’ ambazo mtu amepata kwa alichoweka mtandaoni na hata kwa ujinga (wanaoita kiki) ambao mtu anakuwa amefanya.

Majivuno ambayo watu wanatafuta kwenye vitu hivyo yamekuwa hayawasaidii chochote, zaidi ya kuwapoteza kwa kuhangaika na yasiyokuwa muhimu.

Kama unataka vitu sahihi vya kujivunia navyo, vipo vingi, ambavyo vitakusukuma kuwa bora zaidi na hivyo kuwa na manufaa.
Jivunie kwa kazi unayofanya, kazi ambayo inaongeza thamani kwenye maisha ya wengine. Hapo ona jinsi kile unachofanya kinavyogusa maisha ya wengibe.
Jivunie hatua unazopiga kwenye maendeleo yako binafsi, kimwili, kiakili na kiroho. Ona jinsi ulivyokuwa chini na sasa uko juu, siyo kwa kujilinganisha na wengine, bali kwa kujilinganisha na wewe mwenyewe.
Jivunie misingi ya maisha uliyochagua kuishi, ambayo inakupa mwongozo sahihi na kuweza kujua haraka pale unapokosea na kuweza kujirekebisha.

Kwa kujivunia kwa yale yaliyo sahihi, kunafanya maisha yako yawe na maana kwako na kwa wengine pia.
Na hujivunii kwa kiburi, bali kwa unyenyekevu, ili kupata msukumo wa kuendelea kufanya kilicho sahihi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu msimamo na ung’ang’anizi, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/10/2110

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani