Siku moja nikiwa kliniki, niliona kwenye orodha ya wagonjwa wanaosubiri kuingia kwangu kutibiwa kukiwa na mgonjwa mwenye miaka 93. Kwa haraka nilipata picha atakuwa ni mzee sana, ambaye atakuwa kwenye kiti cha kuendeshwa na atakuwa hawezi kutembea.

Lakini nilipoita mgonjwa huyo, alikuja akiwa anatembea mwenyewe na alionekana kuwa na nguvu za kutosha na alikuwa ameongozana na kijana ambaye ni mjukuu wake. Hata wakati wa mazungumzo, aliweza kujieleza vizuri na kujibu maswali mbalimbali.

Niligundua presha yake iko juu kiasi, hivyo nikahoji kama ana historia ya kuwa na ugonjwa wa presha huko nyumba, akanijibu hajawahi kuwa na presha maisha yake yote. Akaendelea kueleza kwamba huenda presha yake imepanda kwa sababu alikuwa amekasirishwa na wajukuu zake siku hiyo.

Nilimwambia kama ningekuwa wewe, kwa miaka 93 uliyonayo, hakuna yeyote ambaye angeweza kunikasirisha, kwa sababu ningekuwa nawacheka tu, kwa kuwa hawajui lolote. Nilimweleza kwa miaka 93 aliyoishi, amekutana na mambo mengi kiasi kwamba hakuna linaloweza kumsumbua kwa sasa. Alicheka na kukubaliana na mimi, huku akitaja baadhi ya aliyokutana nayo, ikiwa ni kufiwa na mume wake, watoto wake kadhaa na matatizo mengine.

Baada ya kumpatia matibabu na kuondoka, nilitafakari kile nilichomwambia, kwamba kama ningekuwa yeye, yaani kuwa na miaka 93, nisingekasirishwa na yeyote, badala yake ningeishia tu kuwacheka, kwa kuwa hawajui lolote. Nikajiuliza iwapo inahitaji kweli nifikishe miaka 93 ndiyo nianze kufanya hivyo.

Nikaona haihitaji kusubiri mpaka nifike miaka fulani ndiyo niweze kuishi hivyo, nikachagua kuanza kuishi hivyo sasa, kwa kutokuruhusu yeyote anayefanya chochote kinikasirishe au kunivuruga. Inapotokea mtu anafanya hivyo, nitamcheka tu, kwa sababu hajui lolote. Na siyo kwa sababu mimi najua zaidi yake, ila kwa sababu najua sijui, ila yeye anajua anajua ndiyo maana anafanya anavyofanya.

Ujumbe wangu kwako leo rafiki yangu ni huu, kuna namna umekuwa unajiambia utaishi baada ya kupata vitu fulani. Labda unajiambia ukishakuwa na fedha nyingi utaanza kuishi namna fulani. Au ukishakuwa kiongozi utakuwa na maisha ya aina fulani.

Huhitaji kusubiri mpaka upate kile unachotaka ndiyo uanze kuishi kwa namna uliyopanga, badala yake unapaswa kuanza kuishi hivyo sasa. Maana wewe wa sasa kabla hujapata unachotaka, huna tofauti na wewe utakayekuwa ukishapata unachotaka.

Na hakuna hatua moja ya mabadiliko kwamba ukishapata kitu fulani basi unabadilika na kuwa mtu fulani. Kama huwezi kubadilika sasa na kuishi vile unavyotaka, hata ukipata unachotaka hakitakubadilisha, na pia itakuwa vigumu kwako kubadilika maana unakuwa umeshajizamisha kwenye shimo kubwa zaidi.

Huna cha kusubiri, chagua aina ya maisha unayotaka kuishi na anza kuyaishi sasa, hilo litarahisisha wewe kupata kile unachotaka kuliko kusubiri upate unachotaka ndiyo uanze kuishi vile unavyotaka. Kwa kutokuishi maisha unayoyataka kutakuchelewesha kupata unachotaka na hata ukikipata, njia ulizotumia zitakuzuia kuishi maisha unayoyataka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha