Kuna watu wanaamini ushindani ndiyo njia nzuri wa kuwasukuma kufanya makubwa zaidi.

Lakini hilo siyo kweli, ushindani huwa unamfanya mtu asahau kule anakotaka kufika na kuanza kuangalia wengine wanafanya nini ili kuwazidi.

Kinachotokea, hata kama umewashinda wale unaoshindana nao, unakuwa umepoteza, kwa sababu hujawa wewe.

Mafanikio ya kweli hayaletwi na ushindani, bali yanaletwa na utofauti.

Utaweza kufanya makubwa kama utachagua kuwa bora zaidi kila siku na kufanya kitu kuwa bora zaidi ya kilicho sasa.

Kwa kuwa bora zaidi kila siku ni kuhakikisha unaimaliza leo ukiwa tofauti na ulivyoimaliza jana. Ukiwa unajua kitu ambacho jana hukuwa unakijua, ukiwa umejaribu kitu ambacho jana hukujaribu na ukiwa unaamini zaidi kwenye kile unachofanya kuliko ulivyokuwa unaamini jana.

Kwa kila unachogusa, basi kiache kikiwa bora kuliko kilivyokuwa kabla hujakigusa. Kwa kila unachofanya, angalia kikoje sasa na unapomaliza kukifanya uhakikishe kimekuwa bora zaidi ya kilivyo sasa. Haijalishi ni kiwango gani cha ubora au utofauti, wewe fuata msingi huo, kwamba chochote unachogusa, utakiacha kikiwa bora zaidi kuliko awali.

Kwa kuishi kwa msingi huu muhimu, utapiga hatua kubwa sana baada ya muda, huku wengine wakikukimbilia lakini wasikukamate. Kwa kukazana na ubora zaidi huna haja ya kuhofia ushindani, maana wenye mtazamo wa ushindani huwa hawawezi kukazana na ubora, wao wanaangalia wengine wanafanya nini kisha kufanya pia.

Kwa kuwa wewe unabadilika kila mara kwa kuwa bora zaidi, yeyote anayeshindana na wewe hawezi kukufikia, ataendelea kuwa nyuma yako. Wakati wewe leo unafanya tofauti na ulivyofanya jana, mshindani wako anarudia kile ulichofanya jana, sasa hapo unaona wazi nani atazidi kuwa juu ya mwenzake.

Uweke msingi huu kwenye kila eneo la maisha yako na kwa kila unachofanya, siyo kazi na biashara tu, bali yote unayojihusisha nayo. Kwa kufanya hivi utageuza kuwa tabia na matokeo mazuri unayopata kwenye eneo moja yatachochea ufanye vizuri kwenye eneo jingine.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha