Magumu yanapokuja katika maisha ya mtu hufanana na kikwazo cha mwanga katika chumba chenye giza. Ndani ya chumba chenye giza ni rahisi kuanguka, kutoona pakuelekea mpaka pale mwanga utapoweza kukijaza hicho chumba. Mwanga hufanya mambo yawe wazi na njia ya kutoka iweze kupatikanika. James Allen ni moja ya waandishi ambao kupitia ukumbusho wa maandiko yao wameendelea kuishi hadi hivi leo. Karibu vitabu 18 vimeandikwa na yeye vikiwa na lengo kubwa la kumuibua mtu kujifahamu uwezo wake mkubwa uliomo ndani wa kukabiliana na maisha na lolote liwezalo kumtokea.

Kwanza kabisa maisha yetu yalivyo ni matokeo ya mawazo yetu wenyewe yakiambatana na matendo yetu. Ni vile hali zetu za fikra hutuumbia tujione na furaha au huzuni katika tunayopitia katika maisha ambayo kwa asilimia kubwa ni sisi wenyewe tumechagua kuyapa tafsiri ya kufikiri kwetu. Hivyo njia ya furaha na mateso ni vile mtu mwenyewe atakavyoweza kuruhusu kufikiri na kutenda.

Mateso ambayo yanatokea katika maisha yetu ni vile tunavyokaribisha mawazo hasi na hisia hasi kunakoshawishi kuchukua hatua ambazo zinazidi kutuumiza na kutukaribishia mateso zaidi. Binadamu hawezi kujikimbia wala kuikimbia akili yake au mwili wake mwenyewe. Hivyo kwa kila jambo atakaloruhusu kupita katika akili basi mwili utaathirika iwe kwa hasi au chanya.

Kuishi anakosemea mwandishi ni kufikiri kwa usahihi na kutenda kwa usahihi. Kwenda kinyume na hili ndipo ambapo maisha huonekana kuwa mabaya na magumu. Vile uwezavyo kumwona mtu ni jinsi alivyo katika fikra. Hivyo unaweza kusema mtu ni fikra. Na hili halipangani kuwa kila kimtokeacho mtu basi kimeongozwa na sharia ya asili ya kupanda na kuvuna au kisababishi na athari (Law of Cause and Effect). Hivyo mtu asione maajabu katika yoyote yale yamtokeayo asisahau kuwa yeye anaweza kuwa kisababishi cha matokeo anayoyaona kwa chochote.

Kuna nukuu isemayo kuwa kwa kila kitu utakacho kuna gharama ya kulipia. Ukija katika ngazi ya juu ya mtu kama kiumbe wa kiroho pia kuna gharama au thamani ya kuonyesha tabia za kiroho ambazo fedha haziwezi kununua. Matendo ya huruma, upendo, hekima na furaha hubadilishwa na wengine kwa kutoa na kuishi katika tabia hizi. Kadri mtu anavyoweza kukua na kuwa nazo hizi tabia ndivyo anavyoweza kuona mwanga kwa kila tatizo au gumu atakalolipata.

Kukubaliana na asili inavyofanya kazi ni kujiondosha katika mateso na huzuni pale ambapo utaingia katika magonjwa, magumu, maumivu na hata kupoteza watu wa karibu (kifo). Kwa kuwa huwezi kuzuia asili kufanya vitu kukua, kuchoka na kufa. Kadri mtu anavyokubali ukweli huu wa kuwa mtu hana kinga dhidi ya kushambuliwa na hali za ugonjwa, kuzeeka na kufa basi atakavyopitia au kuwaona wengine wakipitia atakubaliana na asili kuwa ni moja ya kitu kilicho nje ya uwezo wake.

Kujitoa kunaumiza maana ni hatua ya kujivua ubinafsi na kujipa nafasi wewe na ukajitoa kwa ajili ya watyu wengine. Ni mtu pekee aliye mkomavu ambaye huona kitendo cha kujitoa si kwa ajili yake ila kwa wengine kama kitu rahisi. Kadri unavyojitoa mwanzoni inaweza kuwa kazi lakini muda upitavyo ndivyo kitendo hiki kinapokuwa kinaweza kuzalisha upendo na maana kubwa ya maisha ya mtu. Kujitoa kunaleta upendo mkuu na hupaisha ngazi ya juu ya utoshelevu.

Kuanguka kote katika tabia hatarishi, uraibu ni zao la usimamizi mbovu wa hisia na mawazo. Kukosa kudhibiti mawazo na hisia ndiko kunakozalisha hatua na maamuzi mabaya yanayomuingiza mtu katika mateso na majuto. Wajibu makini wa kusimamia fikra kwa mtu mwenyewe ni kupunguza mateso yanaweza kuzalishwa na hatua zinazoongozwa na hisia hasi na mawazo mabaya.

Kujizuia ni mlango wa uhuru na maisha yalo salama. Wengi wameingia katika mateso makubwa sababu ya kukosa kujizuia tamaa zao. Maisha ya mtu ambayo yanakosa kujizuia ni maisha yasiyo na kinga yanayoweza kushambuliwa na chochote kile na wakati wowote ule. Mtu huanza kuona yupo huru pale ambapo ataweza kujitawala mwenyewe na kutawala hisia na mawazo yake mwenyewe.

Hekima ni njia kuu ya kuishi kwa furaha na ndipo ilipo furaha kuu ya maisha. Hekima ni ulinzi wa fikra na nafsi ya mtu. Hekima ni kiongozi wa kiasi na hutambua jambo jema na baya. Hekima inapatikana katika utendaji mbali na watu wasemavyo hupatikana kwa kusoma vitabu, kutembea au kusoma falsafa. Utendaji wa mambo katika maisha ndiko kunamtambulisha mtu kuwa huyu ana hekima au mpumbavu. Mwandishi anasema njia ya kuiendea hekima ni wazi japo wengi hukwepa kuiendea na hapo ndipo maisha ya mateso yanapobisha hodi kwao.

Vitu au hali hubadilika ni kazi ya asili. Hakuna kitu au hali hubakia kuwa hivyo daima. Hata fikra nazo huendelea kubadilika kutokana na hali mbalimbali mtu atakazopitia. Watu hukua na kadri anavyopanda ngazi ya juu ndivyo anavyoona madhaifu na makosa mengi ambayo kwa wakati huo kwa kukosa maarifa ya juu alifanya kwa ujinga. Hivyo makosa, udhaifu, mateso na maumivu ni hali ambazo huendelea kumfuatilia mtu maisha yake yote.

Mchambuzi-

Dr.Raymond Nusura Mgeni

raymondpoet@yahoo.com

+255 676 559 211