Wanaotaka mafanikio makubwa ni wengi,

Wanaotaka kuwa na utajiri ni wengi,

Wanaotaka umaarufu ni wengi,

Lakini ni wachache sana wanaopata kile wanachotaka, katika watu 100 ni mmoja pekee anayefikia kile hasa anachotaka.

Siyo kwa sababu watu hao ni wa tofauti sana, ila watu hao wamejitoa zaidi ya wale ambao hawafikii.

Kitu cha kwanza kabisa wanachofanya wale wanaopata wanachotaka ni kujikata wao wenyewe. Wakijua kwamba hawawezi kupata wanachotaka kama watabaki kama walivyokuwa. Hivyo wanabadilika kabisa, wanazaliwa upya.

Wanaachana na kila cha zamani walichokuwa wanafanya, wanaachana na kazi walizokuwa nazo au wakibaki nazo basi wanazifanya kwa utofauti mkubwa. Wanavunja mahusiano mengi waliyokuwa nayo hapo awali, na yale yanayosalia yanakuwa na mchango kwa mafanikio yao.

Wanatoa vitu vingi kafara, vitu vingi wanavyovipenda wanatengana navyo, wanakuwa tayari kuviacha japo inawauma lakini kupata wanachotaka kunawasukuma zaidi.

Wana shauku kubwa ndani yao ya kupata kile wanachotaka, wamejenga mifumo ambayo inawaweka kwenye njia sahihi ya kupata wanachotaka. Hawabahatishi, wanajua wapi wanakwenda na namna gani ya kufika pale.

Hawatafuti njia za mkato, hawasikilizi maoni ya kila mtu na hawahangaiki na vitu vizuri wanavyokutana navyo njiani, wao wanaona kule wanakotaka kufika na macho yao hayatoki hapo.

Unaweza kujipima mwenyewe na kuona kama kweli utapata kile unachotaka, kuona kama kweli umejitoa, kama kweli umejikana na kama kweli kuna vitu umevitoa kafara. Hakuna mafanikio makubwa bila ya vitu hivyo vitatu. KUJITOA, KUJIKANA na KUTOA KAFARA.

Ieleweke vizuri kwenye kutoa kafara haimaanishi uue watu au kufanya kitu cha kujitesa, bali kuwa tayari kuacha kitu unachopenda sana ambacho hakina mchango kwako kufika unakotaka ili uweze kufanya kilicho sahihi. Kutoa kafara inaweza kuwa kuacha kazi unayoitegemea sana sasa, ili uweke nguvu zako zote kwenye biashara. Inaweza kuwa kuvunja mahusiano ambayo umekuwa nayo kwa muda mrefu lakini yanakuwa kikwazo kwako. Ni nini unapenda sana sasa lakini kinakukwamisha kufika unakotaka kufika? Ni wakati sasa wa kukiacha ili nguvu zako ziende kwenye kile kilicho sahihi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha