“When you approach a man, you should think not about how he can help you, but how you might serve and help him.” – Leo Tolstoy

Mara nyingi unapokutana na mtu huwa unaangalia anawezaje kukusaidia badala ya kuangalia unawezaje kumhudumia.
Hata kwenye kazi na biashara, unaangalia nini unachopata na siyo nini unachotoa.
Mtazamo huu ndiyo chanzo cha wengi kutokufanikiwa.

Unapoangalia nini unapata, unajiwekea ukomo kwenye nini ufanye.
Utafanya yale tu yanayokulipa, utajihusisha na wale wanaokunufaisha.
Hivyo utafanya kwa uchache na utajihusisha na watu wachache.

Mtazamo sahihi na utakaokuwezesha kufanikiwa ni kuangalia unatoa nini badala ya unapata nini.
Kuangalia unawahudumiaje wengine badala ya kuangalia wanakusaidiaje.

Unapoangalia nini unatoa, unaondoa ukomo wowote kwenye kile unachofanya na wale unaojihusisha nao.
Kwa kanuni ya asili, kila unachofanya kitalipwa, inaweza isiwe leo lakini lazima utalipwa.
Hivyo acha kuangalia unapata nini, bali anza kuangalia unatoa nini.
Acha kuangalia unasaidiwaje na anza kuangalia unawahudumiaje wengine.
Kadiri unavyotoa kwa wengine, ndivyo unavyopata zaidi.

Asubuhi ya leo tafakari ni yapi unayotoa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla.
Tafakari ni eneo lipi unalohudumu, ni kwa namna gani watu wananufaika kupitia wewe na kisha weka mkazo kwenye hayo.
Utasukumwa kutoa zaidi na hilo litakuweka kwenye nafasi ya kupata zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu gharama ya ziada utakayolipa, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/19/2119

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.