Watu wengi huwa wanaendesha maisha yao kwa hisia, kwa kufuata mihemko yao.

Ndiyo maana wengi hawawezi kufanya maamuzi na kuyasimamia kwa muda mrefu.

Ni sawa na mtu anayeenda kwenye mkutano wa hamasa au kusoma kitabu cha hamasa, anahamasika sana na kutoka akiwa anajiambia anakwenda kubadilika na kufanya makubwa.

Lakini anapolala na kuamka siku inayofuatia, anakuwa ameshaachana kabisa na maamuzi aliyokuwa amefanya. Anakuwa amerudi kwenye maisha yake ya awali.

Kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, uka kazi kubwa mbili za kufanya.

Kazi ya kwanza ni kudhibiti hisia na mihemko yako mwenyewe. Na hapa siyo kuzizuia, maana huwezi, badala yake kuepuka kufanya maamuzi kwa hisia na mihemko. Pale unapogundua kwamba hisia zipo juu, jipe muda kwanza hisia zishuke, fikiria kuhusu jambo kwa kina na ndipo ufanye maamuzi.

Kazi ya pili ambayo ni kubwa zaidi na wengi huwa wanaishindwa ni kujikinga na mihemko ya wengine, kutengeneza mfumo wa maisha yako kwa namna ambayo mihemko ya wengine haiwezi kukudhuru. Tunashirikiana na watu wengi kwenye maisha, sasa tunaporuhusu maamuzi ya watu hao kuweza kuathiri sana maisha yetu, tunajiweka kwenye hatari ya kuvurugwa na mihemko yao.

Chukulia mfano umeajiriwa na njia pekee unayotegemea ya kukuingizia kipato ni ajira hiyo. Siku ya Ijumaa jioni mwajiri wako anakuambia Jumatatu atakuwa na kikao muhimu na wewe, hivyo usikikose. Hakuambii kikao kinahusu nini, ila hakuwa kwenye uso wa furaha wakati anakueleza hilo.

Sasa hebu niambie kama huo mwisho wa wiki utakuwa mzuri kwako. Hata kama kuna mambo mazuri uliyokuwa umepanga kufanya mwisho wa wiki, hutayafurahia, mawazo yako yote yapo kwenye jumatatu, nini kinakwenda kutokea. Unaanza kupata mpaka picha labda anataka kukufukuza kazi, na hapo unaanza kupata picha maisha yako yataendaje.

Unazipoteza siku mbili za maisha yako, kwa sababu ya kitu kinachokuja kutokea baadaye, ambacho hata hujui ni nini. Yote hiyo ni kwa sababu umeruhusu mihemko ya wengine iweze kuvuruga maisha yako. Umeruhusu maamuzi anayoweza kufanya mtu mmoja yawe na uwezo wa kupindua kabisa maisha yako. Na unalipa hilo kwa maumivu na kukosa uhakika.

Kama unataka kufanikiwa na uwe na utulivu wa moyo wako, ondoa kila aina ya nafasi uliyotoa kwa wengine kuweza kuvuruga maisha yako. Hata kama ni wema kiasi gani, hata kama wamekupa uhakika kiasi gani, ndani yako hakikisha una kitu cha kusimamia, ambapo hutaweza kuvurugwa na mihemko ya mtu yeyote yule.

Hili linawezekana sana pale unapokuwa umejitambua, unapokuwa unajua nini mchango wako kwa wengine na unapokuwa umejijengea njia mbadala za kupunguza utegemezi wako kwa mtu mmoja au kitu kimoja.

Mihemko, iwe ni yako au ya wengine ni mibaya, yakinge maisha yako na kila aina ya mhemko.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha