Do not be concerned too much with what will happen. Everything which happens will be good and useful for you. — Epictetus

Mtu mmoja alipotelewa na farasi aliyekuwa anamtegemea sana, majirani zake wakaja kumpa pole kwa upotevu huo.
Siku chache baadaye farasi aliyepotea akarudi akiwa na farasi wengine wawili wa mwituni, majirani wakaja kumpa pongezi kwa farasi hao.
Kijana wake akiwa anajaribu kupanda farasi wa mwituni, akaanguka na kuumia, majirani wakaja kumpa pole kwa kijana kuumia.
Kesho yake wakapita watu kuchukua vijana wa kujiunga na jeshi na kwenda kwenye mapigano, kijana aliyekuwa ameumia hakuchukuliwa. Majirani wakaja kumpongeza kwa hilo.

Tuna tabia ya kukimbilia kuyaweka yanayotokea kwenye kundi la MAZURI au MABAYA.
Lakini ukweli ni uzuri au ubaya wa kitu ni tafsiri zetu tu, mambo huwa yanatokea.
Tuna tabia ya kujiambia kila jambo huwa linatokea kwa sababu, lakini hiyo bado ni tafsiri yetu wenyewe, mambo hutokea kama yanavyotokea.

Ukweli ni kila jambo linalotokea kwenye maisha yako, lina matumizi kwako.
Hivyo acha kukimbilia kusema ni zuri au baya,
Acha kutafuta kujifariji kwa kusema limetokea kwa sababu njema,
Bali jiulize unawezaje kulitumia?

Ukijiuliza swali hilo kwa kila linalotokea kwenye maisha yako, utapiga hatua kubwa sana, utaziona fursa nyingi zinazokuja na kila kinachotokea kwenye maisha yako.

Asubuhi ya leo tafakari ni mambo gani ulikuwa unayahofia sana huko nyuma, ila baadaye yakatokea na hayakuwa mabaya kama ulivyohofia? Ona jinsi ulivyoweza kuyatumia vizuri na ukanufaika.
Labda ulikuwa unahofia kukosa kazi, ukakosa na hilo likakuwezesha kuwa kwenye biashara.
Labda ulikuwa unahofia mahusiano kuvunjika, yakavunjika na ukaweza kujenga mahusiano mengine bora zaidi.
Tafakari na utaona mengi.
Na kuanzia sasa, usihifie chochote ambacho hakijatokea, jua utaweza kukitumia vizuri.
Na kwa kila kinachotokea kwenye maisha yako, jiulize unawezaje kukitumia vizuri na maisha yako yatanufaika sana.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kazi na mbwembwe, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/20/2120

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.