Upo usemi wa Kiswahili kwamba mtembea bure siyo sawa na mkaa bure, maana yule anayetembea bure anaweza kukutana na fursa ambazo anayekaa mahali pamoja bure hawezi kuzipata.
Kauli hii inahusika kwenye maeneo mengi ya maisha yetu, ikiwepo kazi zetu mbalimbali.
Mtazamo mkuu tulionao kwenye shughuli mbalimbali tunazofanya ni kulipwa kadiri ya tunavyofanya, kuthaminisha mchango wetu na kutaka watu watulipe hivyo. Hakuna ubaya kwenye hilo, lakini linakuwa kikwazo pale ambapo hakuna anayejua unaweza kufanya nini.
Unapokuwa mgeni kwenye eneo fulani au kwenye kile unachofanya, watu hawawezi kujua thamani yako halisi na hivyo hawatakuwa tayari kukulipa kwa kadiri unavyotaka wewe mwenyewe. Hivyo ukisubiri mpaka upate wa kukulipa kama utakavyo, utakaa bila ya kitu cha kufanya kwa muda mrefu na hapo utazidi kujipoteza.
Kwa mwanzoni itakupasa ukubali kulipwa kiwango kidogo au hata kufanya bure kabisa, lengo lako wakati huo ni kuonesha thamani yako, kuonesha namba ambavyo una mchango mkubwa na kuhakikisha watu wanakuwa na utegemezi kwako kiasi kwamba hawatakutaka uondoke.
Ni baada ya kutengeneza thamani na utegemezi huo ndipo sasa unaweza kudai kulipwa thamani halisi kulingana na thamani kubwa ambayo tayari umeshaitoa.
Pale unapokosa nafasi ya kufanyia kazi kile ulichonacho kwa sababu hakuna aliye tayari kukulipa thamani yako, chagua kufanya bure kile unachoweza ili kuonesha thamani kubwa uliyonayo. Unapofanya bure, usifanye kwa mazoea kabisa, badala yake jisukume kufanya kwa utofauti mkubwa na zalisha matokeo ambayo ni bora kabisa.
Uzuri wa kufanya hata kama ni bure unazidi kuwa bora, unajulikana na kukuza mtandao wako. Kutokufanya kabisa kunakupoteza kwa sababu hujifunzi mapya na pia hakuna anayekujua.
Japo kufanya bure kunaweza kufanya watu wasithamini kile ulichonacho, lakini ukiweza kutoa thamani kubwa kuliko walivyotegemea au kuzoea, thamani yako kwao itakuwa mara dufu.
Uzuri ni kwamba, asili huwa inajiendesha kwa kanuni zake, huwa inalipa kila thamani inayozalishwa. Hivyo hata kama unayemfanyia bure hathamini na kukulipa, kuna wengine wataona thamani unayotoa na watakuwa tayari kukulipa unachostahili.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Makala nzuri sana ya kutupa moyo wa kuendelea kufanya kile tulichoamua kufanya hata kama hakuna matokeo tunayoona kwa sasa.
Asante sana kocha.
LikeLike
Karibu.
LikeLike