Nina rafiki yangu mmoja ambaye tunajuana kwa karibu miaka kumi sasa. Ni rafiki ambaye haipiti muda sijakutana naye na mara nyingi huwa ni kwa kutembelea ofisi yake.

Siku za karibuni, amepata rafiki mwingine ambaye wanashirikiana naye kwenye ofisi yake. Hivyo ninapoenda pale ofisini kwa rafiki yangu, nakutana na huyo mwingine ambaye wanashirikiana naye na tunakuwa na mazungumzo mbalimbali.

Siku moja nikaenda ofisini hapo, sikumkuta rafiki yangu, ila nikamkuta yule anayeshirikiana naye sasa. Katika mazungumzo akaniuliza uliwezaje kuwa na urafiki na huyu, mbona hamuendani kabisa?

Akawa ananieleza mambo aliyoyajua kuhusu huyo rafiki yangu kwa miezi michache ambayo amefanya naye kazi, ni vitu ambavyo hakuvijua awali. Alitaka kuendelea kueleza zaidi lakini nikamjibu nayajua yote hayo hivyo haina haja.

Kutokana na mazungumzo hayo mafupi nilitafakari hilo maana sikuwahi kulipa uzito sana. Na kuna mafunzo makubwa matatu ambayo napenda nikushirikishe hapa;

Funzo la kwanza ni kuhusu tabia zetu, huwa zinasema kwa sauti kuliko maneno yetu. Hivyo tunaweza kusema tutakavyo, lakini tabia zetu zitaeleza wazi. Matendo yetu yana nguvu kuliko maneno hivyo tunapaswa kuwa makini sana na matendo yetu.

Funzo la pili ni kuhusu mahusiano, lengo la kuwa kwenye mahusiano na mtu yeyote yule siyo kumbadili awe kama unavyotaka wewe, bali kumkubali kama alivyo. Wengi hukosea pale wanapoingia kwenye mahusiano wakiamini wanakwenda kuwabadili wale wanaojihusisha nao, hilo huwa halitokei na mahusiano huwa na misukosuko. Unapokubali kuwa na mahusiano na mtu, jua ni kipi unanufaika nacho kutoka kwake na angalia kama kina manufaa kuliko udhaifu alionao. Usijidanganye utakwenda kumbadili.

Funzo la tatu ni kujua udhaifu wa yule uliyenaye kwenye mahusiano uko wapi na kuuepuka ili msisumbuane. Kwa mfano kwa huyo rafiki, miaka ya nyuma nilitaka kushirikiana naye kwenye biashara, kulikuwa na fursa nzuri iliyojitokeza, lakini sikuwa na uhakika sana. Hivyo nikamwambia aendelee na rafiki mwingine na baadaye nitaungana nao. Hawakuishia vizuri na kikubwa kilichochangia ni udhaifu ambao rafiki huyu tunayemzungumzia hapa anao. Hivyo nikawa nimejifunza ni mambo gani naweza kushirikiana naye na yapi siwezi kushirikiana naye. Kwa namna hiyo, tumekuwa hatusumbuani.

Jua kila unachofanya watu wanaona, wanaweza wasikuambie lakini watakuhukumu kwa matendo yako kuliko maneno yako. Na unapochagua kuwa na mahusiano na mtu, jua uimara wake na madhaifu yake na kama unamkubali, basi mkubali kama alivyo na siyo kujiambia unakwenda kumbadili.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha