Ukiwaangalia dagaa na kuwalinganisha na samaki wengine wakubwa, unaweza kufikiri dagaa ni watoto wa samaki, ambao kama wangeachwa basi wangekuja kuwa samaki wakubwa.

Lakini huo siyo ukweli, dagaa ni jamii ya samaki ambao ni wadogo, hivyo unapomuona dagaa ni samaki aliyekamilika, hata aachwe kiasi gani, hatafikia ukubwa wa samaki wengine wakubwa.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye biashara.

Watu wengi hufikiri biashara ndogo ni biashara kubwa ambazo hazijakua na kwamba zikiendelea zinaweza kuwa kubwa.

Na hiyo ndiyo sababu kwa nini wafanyabiashara wanaojaribu kukuza biashara zao ndogo huwa zinaishia kufa. Ni kwa sababu hawajui kwamba biashara ndogo ni aina tofauti kabisa ya biashara ambayo huwezi kuilinganisha na biashara kubwa.

Biashara kubwa na biashara ndogo zinatofautiana kabisa kwenye uendeshaji wake na mafanikio yake.

Hivyo kama mfanyabiashara unapaswa upo au unataka kuwa kwenye biashara ya aina gani, kubwa au ndogo.

Biashara ndogo ina manufaa makubwa ya udhibiti wa mtu mmoja, hivyo maamuzi yanaweza kufanyika haraka na kunufaika na fursa mbalimbali. Pia inakuwa na ukaribu zaidi na mteja na kuweza kumpa huduma ya kipekee na kuweza kutoza gharama kubwa zaidi. Lakini biashara hizi zinakosa nguvu ya ukubwa wa kutawala sehemu kubwa ya soko.

Biashara kubwa ina manufaa ya kutumia ukubwa wake kuwafikia wengi na hivyo kuweza kutoza gharama ndogo na kutengeneza faida kwa wingi wa wateja. Lakini huwa zinakosa uharaka wa kufanya maamuzi na kushindwa kumhudumia mteja kwa upekee wake.

Kama tulivyoona, kila aina ya biashara ina uimara na madhaifu yake, chagua unataka kuwa kwenye biashara ipi na kazana na uimara wa aina hiyo ya biashara badala ya udhaifu wake.

Kama upo kwenye biashara ndogo, usijaribu kuigiza kama biashara kubwa, kwa sababu utashindwa kwenye zote. Kumbuka hili, dagaa siyo watoto wa samaki wakubwa bali ni jamii tofauti ya samaki.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha