“There are persons whose only merit consists in saying and doing stupid things at the right time, and who ruin all if they change their manners.” – Johann Wolfgang von Goethe

Kuna watu ambao wamepata umaarufu mkubwa kwa kufanya mambo ya kijinga na ya hovyo kabisa.
Hasa kwenye zama hizi za mtandao, hakuna njia rahisi ya kupata umaarufu wa haraka kama kufanya mambo ya kijinga.
Kama unataka nchi nzima ikujue, vujisha picha zako za uchi mtandaoni, au anza kuwashambulia watu kwa kuwatukana na kuwadhalilisha bila sababu yoyote.
Kuna watu wanafanya hivyo na wanaupata huo umaarufu kweli.
Na hawawezi kuacha kufanya hivyo, maana hawana kingine cha kuwafanya wajulikane.

Kinachotokea ni kwamba umaarufu wa aina hii, unamsukuma mtu kuendelea kufanya ujinga zaidi ili aendelee kuongelewa zaidi.
Kwa kuwa ni rahisi kufanya ujinga na wengi wapo tayari kwa hilo, ushindani unakuwa mkali.
Haishangazi kwa nini mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya kusambaza kila aina ya sumu na ujinga.

Asubuhi hii tafakari ni nini hasa unachotaka kwenye maisha yako
Unachotaka ni maisha hayo yawe bora au unachotaka ni umaarufu wa haraka?
Kama unataka umaarufu wa haraka, jua huwezi kuupata pamoja na maisha bora.
Hutaupata pamoja na utulivu wa ndani.
Utalazimika kufanya mambo ya kijinga na ambayo baadaye yatakuwa kikwazo kwako.
Tambua kwamba mtandao wa intaneti huwa hausahau, chochote unachoweka mtandaoni kinahifadhiwa milele, hata kama utakifuta.
Hivyo kuwa makini, jua kile unachotaka na fanyia kazi hicho kwa usahihi.

Kuna wakati utaona kama wale wanaofanya mambo ya kijinga wanapata umaarufu kuliko wewe, wanapata fursa nzuri ambazo wewe hupati.
Utaona labda ni wakati wa wewe kufanya hivyo pia.
Lakini usikubali kamwe kufanya hivyo.
Mara zote fanya kile kilicho sahihi, hutapata umaarufu wa haraka, lakini utakuwa na maisha bora na tulivu.

Na pia isiwe kazi yako kuangalia nani kafanya nini na kapata nini.
Isiwe kazi yako kutaka kila mtu afanye kile unachoona ni sahihi.
Kuna watu ambao tayari wameshajijenga kwenye ujinga kiasi kwamba wakiuacha watapotea haraka, hivyo huona ni bora wapotee kidogo kidogo kwa kuendelea na ujinga wao.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu kutafuta sababu za kushindwa, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/25/2125

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.