“Life will only change when you become more committed to your dreams than you are to your comfort zone.” – Bill Cox
Maisha yako yatabadilika pale utakapojitoa zaidi kwa ajili ya ndoto zako kubwa kuliko kujitoa zaidi kwenye mazoea.
Vita ya kwanza na kubwa kabisa unayopaswa kuishinda ni kuachana na mazoea uliyonayo sasa.
Maana hata upange kufanya makubwa kiasi gani, ni rahisi sana kurudi kwenye mazoea.
Hivyo kitakachobadili maisha yako ni wewe kuakua kwa dhati na kuwa na msimamo kwamba unaachana na mazoea.
Haijalishi ulichopanga kufanya kinakuwa kigumu kiasi gani, haijalishi mazoea yanakuvutia kiasi gani,
Pale unapokataa kurudi kwenye mazoea na kuchagua kuendelea na mipango uliyojiwekea, ndipo maisha yako hubadilika.
Mabadiliko yangekuwa yanatokea kwa matamko na mipango, kila mtu angekuwa amefanikiwa sana.
Lakini mambo hayaendi hivyo.
Wengi hujipa matamko ya kubadilika.
Wengi hupanga kubadilika.
Lakini unapofika wakati wa utekelezaji wa mipango ambayo mtu amejiwekea, ushawishi wa kurudi kwenye mazoea unakuwa mkubwa.
Asubuhi ya leo tafakari ni mara ngapi umepanga kubadilika kwenye maisha yako.
Mara ngapi umefikiria ndoto na mipango mikubwa uliyonayo na kujiambia unakwenda kuifanyia kazi.
Lakini siku chache baadaye unajikuta umeachana nayo na kurudi kwenye mazoea.
Kila mmoja wetu ameshapitia hili mara nyingi,
Siyo udhaifu bali ndiyo ubinadamu.
Na kama unataka kuuvuka, lazima uamue kweli kwamba unachotaka ni kufikia ndoto yako, liwake jua, inyeshe mvua hakuna kitakachokuzuia.
Lazima ujiwekee kiapo chako mwenyewe kwamba kwenye haya maisha utafikia ndoto yako kubwa au utakufa ukiwa unapambana. Hutaruhusu kabisa kurudi kwenye mazoea.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu dagaa siyo watoto wa samaki, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/10/26/2126
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.