Umekuwa unasikia takwimu mbalimbali za nafasi ya mtu kufanikiwa.
Watu kwenye jamii wamegawanywa kwenye makundi makubwa mawili, asilimia 1 ambao wamefanikiwa sana na asilimia 99 ambao hawajafanikiwa.
Takwimu hizo ni za kweli pale unapoiangalia jamii na zinaleta picha ambayo inafanana kwenye maeneo mengi.
Lakini kwako wewe, takwimu na nafasi hizo siyo sahihi, hivyo hupaswi kuziamini.
Nafasi ya wewe kufanikiwa siyo 99 kwa 1, kali 50 kwa 50.
Yaani kuna asilimia 50 ya kufanikiwa na asilimia 50 ya kushindwa. Kama ilivyo kwenye kurusha shilingi, nafasi ya kupata kichwa ni 50 kwa 50.
Hivyo kuanzia sasa fikiria kwa takwimu hizi mpya, kwamba nafasi ya wewe kufanikiwa ni asilimia 50, yaani utafanikiwa au hutafanikiwa.
Utafanikiwa pale utakapojua unachotaka, utakapojitoa kukipata na utakapokuwa king’ang’anizi na kutokukubali ukwamishwe na chochote.
Utashindwa pale utakapokuwa hujui unachotaka na unapokuwa hujajitoa kweli kufanikiwa.
Kwa kujua takwimu hizi mpya, inakuondolea ukomo wa kifikra ambao wengi wamejiwekea, kwa kufikiri mafanikio ni ya wachache walio na fursa fulani ambazo wengine hawana.
Kila fursa unayohitaji ili kufanikiwa tayari unayo, ni wewe uzitambue na kuzitumia na kufanikiwa au usizijue na usifanikiwe. Ni hamsini kwa hamsini, hamna tofauti na hapo.
Unajua jinsi akili yako ilivyo na nguvu, kile unachoamini ndiyo kinachotokea, hivyo kuwa na imani kubwa kwenye mafanikio yako, yafanyie kazi na hatimaye utayafikia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,