“Miaka mitano ijayo utakuwa sawa na ulivyo leo, isipokuwa kwa watu utakaokutana nao na vitabu utakavyosoma.” ― Charlie Tremendous Jones

Rafiki yangu mpendwa,

Leo tarehe 28/10/2020 ni siku ya kipekee kwenye maisha ya kila Mtanzania, kwani tunapata nafasi ya kwenda kushiriki kuamua ni watu gani wa kutuongoza kwa miaka mitano ijayo.

Hili ni tukio ambalo huwa linatokea mara moja kila baada ya miaka mitano na maamuzi tunayofanya tunakaa nayo kwa kipindi hicho cha miaka mitano.

Kwenye ujumbe wa leo nina mambo mawili; jambo la kwanza ni kukusihi ukapige kura leo na jambo la pili ni mtu muhimu unayepaswa kumchagua leo ambaye atayabadili maisha yako kwa uhakika.

Tuanze na umuhimu wa kupiga kura leo.

Kama wewe ni Mtanzania mwenye umri zaidi ya miaka 18 na umejiandikisha kupiga kura, basi leo nenda kapige kura. Huna sababu yoyote kwa nini usipige kura yako siku ya leo.

Hivyo nikuombe sana rafiki yangu, nenda kapige kura, mimi nakwenda kupiga kura mapema na wewe fanya hivyo. Ni haki yetu na ushiriki wetu kwenye kufanya maamuzi ya namna gani taifa letu liongozwe.

Kuna sababu za kijinga nyingi ambazo watu wamekuwa wanazitumia kujihalalishia kutokupiga kura, leo nakwenda kuvunja sababu kubwa tatu zinazotumiwa sana.

Sababu kwa kwanza; sina muda wa kupoteza.

Wapo wanaosema hawana muda wa kupoteza kwenda kupanga foleni kupiga kura, ni bora watumie muda huo kwenda kutafuta pesa au kufanya yao mengine.

Rafiki, hii siyo tu sababu ya kijinga, bali ni ya hovyo mno. Uchaguzi unatokea mara moja ndani ya miaka mitano, hata kama utapoteza simu moja, ni moja kati ya siku 1825. Sasa hebu niambie tangu mwaka 2015 mpaka leo ni siku ngapi umezipoteza bila ya kufanya chochote. Hata huko ni mbali, tuangalie tu mwaka huu 2020, ni siku ngapi umeipoteza kwa mambo yasiyo na msingi? Usitumie sababu hii, nenda kapige kura, hupotezi chochote ambacho hujawahi kupoteza siku za nyuma.

Sababu ya pili; ninayemkubali atashinda hata nisipompigia kura.

Wapo ambao wanaona kwa sababu upande wanaoukubali una nguvu ya kushinda, basi hawana haja ya kupiga kura, kwa sababu hata wasipopiga, upande huo utashinda.

Rafiki, hata kama upande unaoupigia kura unaona utashinda, kura yako bado inatoa ujumbe kwa upande huo, kuonesha kwamba unauunga mkono na hivyo kujua unawakilisha watu sahihi.

Sababu ya tatu; ninayemkubali hawezi kushinda hivyo nikipiga kura ni kuipoteza.

Wapo ambao wanaona upande wanaoukubali hauwezi kushinda, hivyo hata wakienda kupiga kura ni kuipoteza kura hiyo maana haitaleta ushindi.

Rafiki, kura unayopiga siyo kwa sababu ya mtu kushinda au kushindwa, bali ni kuonesha msimamo wako, unasimamia upande upi. Hivyo hata kama upande ulioupigia umeshindwa, upande unaoshinda unakuwa umepata funzo, kwamba kuna wananchi hawakubaliani na kile wanachosimamia. Hiyo inafanya upande huo kutafuta njia za kuwahudumia wananchi wote, hata wale wasiokubaliana nao.

Kama hutaenda kupiga kura kwa sababu upande unaoukubali haushindi, utawaacha wale wanaoukubali upande unaoshinda wapige kura, anayeshinda ataona anakubalika na wote, kumbe kuna ambao hawamkubali. Hivyo kapige kura, kura yako imebeba ujumbe mzito kuliko tu kuamua ushindi.

Kwa hayo machache rafiki yangu, nikusihi sana uende ukapige kura leo, ni tukio ambalo halitatokea tena mpaka miaka mitano ipite, usipoteze nafasi hii ya kushiriki kwenye demokrasia na kutuma ujumbe wako ni wapi unasimama.

Mtu muhimu unayepaswa kumchagua leo kama unataka maisha yako yabadilike.

Rafiki, najua kampeni za kuomba nani achaguliwe zimefungwa jana. Lakini leo nataka nimpigie kampeni mtu mmoja ambaye hayuko kwenye karatasi za kupigia kura unazokwenda kukutana nazo, ila ana nguvu kubwa ya kuyabadili maisha yako.

Huyu ni mgombea ambaye akikupa ahadi zake, una uwezo wa kumfuatilia na akazitekeleza, siyo mwanasiasa wa kukuambia kuna mchakato na upembuzi yakinifu. Una uwezo wa kumkamata wakati wowote na kumhoji ahadi zake na utekelezaji wake.

Kumwona mgombea huyo, nenda mbele ya kioo, kama una kioo kikubwa kasimame mbele ya kioo hicho, kama una kioo kidogo kishike na kukitazama.

Ile sura unayoiona kwenye kioo, ndiye mgombea wa kwanza unayepaswa kumpigia kura leo hii, kabla hujatoka kwenda kuchagua wagombea wengine.

Utaratibu wa kumpigia kura mgombea huyo ni kwa kutumia kauli hii; “Mimi …… (taja jina lako) nimejichagua kuwa kiongozi mkuu wa maisha yangu, maisha yangu ni jukumu langu na nitachukua hatua kuhakikisha yanakuwa bora. Kila siku nitakazana kuwa bora zaidi ya nilivyokuwa jana, kila siku nitajifunza kitu kipya na nitajituma kwa kwenda hatua ya ziada kwenye kila ninachofanya. Kila siku nitakazana kukuza kipato changu zaidi kwa kukazana kutoa thamani kubwa zaidi kwenye kile ninachofanya. Kwa kila kipato ninachoingiza, asilimia 10 nitajilipa mimi mwenyewe kwa kuweka akiba sehemu ambayo siwezi kuitumia na baadaye nitawekeza akiba hiyo ili izalishe zaidi. Kila kinachotokea kwenye maisha yangu nitakitumia kwa manufaa zaidi, sitalalamika wala kumlaumu yeyote, kama kuna kitu sikipendi nitakibadili na kama siwezi kukibadili nitaachana nacho. Haya ndiyo maisha niliyochagua kuyaishi kwa miaka mitano ijayo na kila siku nitajikumbusha hili kabla ya kuanza siku yangu.”

Chapisha kauli hiyo na iwekee sahihi na kuiweka sehemu ambayo kila siku unaweza kuisoma kabla hujaianza siku yako. Unaweza kupakua nakala ya kuchapisha kwa kubonyeza maandishi haya.

Miaka mitano ijayo.

Rafiki, kwa kumalizia nirudi kwenye nukuu ya Charlie Tremendous Jones niliyoanza nayo makala hii, ambayo inasema; “Miaka mitano ijayo utakuwa sawa na ulivyo leo, isipokuwa kwa watu utakaokutana nao na vitabu utakavyosoma.”

Hapa sihitaji kukushawishi sana kuhusu ukweli wa kauli hii, kwani ninachotaka ufanye ni kujilinganisha ulivyo leo Oktoba 2020 na ulivyokuwa Oktoba 2015. Kama kuna chochote kimebadilika kwenye maisha yako, basi utaona wazi mabadiliko hayo yamechochewa na vitu viwili; maarifa uliyoyapata kupitia usomaji wa vitabu na watu uliokutana nao kupitia njia mbalimbali za kukuza mtandao wako.

Sasa nakupa nafasi ya kupanga miaka mingine mitano itakuwaje kwenye maisha yako, nataka sasa miaka mitano ijayo, yaani 2020 mpaka 2025 ukayajenge maisha yako kwa vile unavyotaka wewe badala ya kusubiri mambo yatokee kwa ajali.

Kukamilisha hilo, kuna nafasi kubwa mbili ambazo nakupa;

Nafasi ya kwanza ni kujiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, hii ni channel ambayo inakupa uchambuzi wa vitabu mbalimbali ya mafanikio na maendeleo binafsi. Kwa kuwa ndani ya channel hiyo, utapata vitabu vizuri vya kusoma pamoja na chambuzi zake. Hivyo kwa miaka mitano ijayo, unakuwa na uhakika wa kupata maarifa sahihi na bora kwa maisha yako. Kujiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Nafasi ya pili ni kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, hii ni programu ya mafunzo na ukocha ninayoiendesha, ambayo pamoja na maarifa mengi na mazuri utakayoyapata, unapata nafasi ya kukutana na watu wengine ambao wana mtazamo wa mafanikio na wanapambana kufikia mafanikio makubwa. Kama pale ulipo sasa umezungukwa na watu wa kawaida, utabaki kuwa kawaida, kama umezungukwa na waliokata tamaa, utakata tamaa. Ukiwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unazungukwa na watu wenye hamasa kubwa ya mafanikio na wanaoamini wanaweza kufanya makubwa, kitu kitakachokusukuma kufanya makubwa pia. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA na utatumiwa maelekezo.

Karibu sana rafiki yangu, karibu twende pamoja kwenye miaka mingine mitano ambayo umejichagua wewe mwenyewe, upate maarifa sahihi kila siku na kuzungukwa na watu sahihi na miaka mitano ijayo, utaiangalia na kuishukuru sana siku ya leo.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata makala zaidi tembelea www.amkamtanzania.com na www.kisimachamaarifa.co.tz