Kila mtu ana madhaifu yake, lakini siyo wote ambao wanayajua madhaifu waliyonayo, kwa sababu wengi hawajapata nafasi ya kujitambua vizuri wao wenyewe.
Kwa wale wanaoyajua madhaifu yao hilo limekuwa haliwasaidii, kwa sababu huchukua hatua moja kati ya hizi;
Hujaribu kuyaficha madhaifu hayo kwa sababu hawataki yaonekane na wengine na kutumiwa kuwaumiza zaidi.
Au wanajaribu kuyaondoa madhaifu yao, kwa kukazana kuwa imara kwenye yale maeneo ambayo wana udhaifu.
Njia zote hizo mbili zimekuwa siyo sahihi, kwani unapoyaficha madhaifu hunufaiki nayo na unapojaribu kuyaboresha unayafanya kuwa na nguvu zaidi.
Namna pekee ya kukabiliana na madhaifu yako ni kuyatambua, kuyakubali na kisha kuyatumia kwa manufaa kwako.
Udhaifu wowote ulionao, una uimara ndani yake, ambao unaweza kuutumia vizuri na ukanufaika sana.
Njia moja kubwa ya kutumia madhaifu yako kwa manufaa kwako ni kutokuyaruhusu yawe kikwazo kwako, kwa kuhakikisha unatumia uimara wako kuziba pengo la madhaifu yako. Hapo hukazani kuyabadili madhaifu yako, bali unatumia uimara wako kuziba pengo linalokuwepo.
Njia nyingine ni kuchagua watu sahihi wa kushirikiana nao, wanapaswa kuwa wale ambao wana uimara kwenye maeneo uliyo na madhaifu. Ukishirikiana na wale ambao wana uimara kwama wako na madhaifu kama yako, kila wakati mtajikuta mnakwazana, kwa sababu mnashindana kwenye kitu kimoja na kuanguka kwenye kimoja. Lakini unaposhirikiana na mwenye uimara pale ulipo na madhaifu na yeye ana madhaifu kwenye uimara wako, mtakwenda vizuri kwa sababu mnategemeana.
Njia nyingine ni kuweka madhaifu yako wazi kwa wengine badala ya kuyaficha, hilo lina manufaa makubwa mawili. Kwanza ni watu kujua nini wanapata kwako na nini wanakosa kwako, huna haja ya kuigiza kitu usichokuwa na hilo linakuweka huru. Pili ni watu kukuchukulia poa, kuna watu kwa kujua madhaifu yako watakuchukulia poa na kutokukupa uzito sana, hilo litakupa wewe nafasi ya kufanya makubwa bila ya kusumbuliwa na baadhi ya watu.
Kila udhaifu ulionao una uimara ndani yake, tambua madhaifu yako, jua uimara ulio ndani ya madhaifu hayo na utumie ili uweze kupiga hatua zaidi.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,