Epuka sana mabishano yoyote yanayohusisha hisia, maana hata kama utashinda kwa hoja, bado hisia za uliyemshinda hazitakuwa zimebadilika, badala yake atakuwa ameimarika zaidi kwenye upande anaosimamia.

Iwe ni kwenye mambo ya imani, mapenzi, michezo, siasa na mengine yoyote yale ambayo watu wameweka imani zao, mabishano au mashindano yoyote yale ni kujipotezea muda wako.

Hivyo kabla hujaingia kwenye mabishano au mashindano yoyote, jiulize kwanza wale walio upande wa tofauti na wewe nini kinawaweka kwenye upande huo. Kama ni kwa imani tu, basi usijisumbue kubishana au kushindana, hata kama unajua upande wako ndiyo sahihi na hata kama utashinda, ushindi wako utakuwa hewa.

Ukilijua hili, utaepusha migogoro mingi sana kwenye maisha yako. Chukua mfano mabishano mengi ambayo umewahi kuwa nayo na mwenza wako, unaweza kuwa uko upande sahihi kabisa, na ukahakikisha anajua uko upande sahihi, lakini mwisho wa siku unaambulia nini? Hakutakuwa na maelewano mazuri, unaweza kushinda kwa hoja lakini mwenza wako asiwe na furaha, je huo ushindi wako umekupa nini?

Kadhalika kwenye biashara, huenda kuna kitu mteja anaamini tofauti na wewe unahakikisha unamwonesha ukweli ni upi, anakubishia na wewe unampa uthibitisho, unashinda, hanunui na harudi tena kununua kwako, je ushindi wako umekusaidia nini?

Kitu kikubwa cha kujifunza hapa siyo kukubaliana na kila mtu, wala kuwaacha wengine wakuambie wanachotaka, bali ni kupima ukubwa na umuhimu wa jambo husika na kile utakachopoteza iwapo utashinda katika kubishania jambo hilo. Kama kukubaliana na mtu hakuna utakachopoteza, huku kupingana naye kuna kitu utapoteza, basi kubaliana naye.

Kwenye kitabu cha Dunes, Paul Atreides akiwa na mama yake jangwani, wanakutana na watu wa jamii ya Fremen ambao wanawapokea vizuri na kuamini utabiri waliokuwa nao umetimia, kwamba Paul ndiye Mesia anayekuja kuwakomboa. Paul anajua hilo siyo kweli lakini mama yake anamwambia kauli ambayo ina nguvu sana. Anamwambia; ‘waache waamini chochote wanachotaka, la muhimu ni wanatuamini sisi.’

Hii ni kauli unayopaswa kuiandika kwenye akili yako na kuhakikisha huisahau kwa namna yoyote ile. Kila unapotaka kuwabadili watu kile wanachoamini, kumbuka kwamba watu hawabadili imani zao kirahisi, hivyo wajibu wako ni kuhakikisha wanakuamini. Hivyo hata kama wanachoamini siyo sahihi, kama tu wanakuamini wewe, hiyo inatosha, shirikiana nao kwenye hiyo imani waliyonayo kwako.

Usijisumbue kubishana na kushindana na watu wabadili imani zao, hata ukiwashinda kwa hoja, bado utakuwa umewapoteza kwa hisia na hawatabadilika, badala yake wataimarisha imani yao zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha