Wakati wa zama za viwanda, kazi zilipimwa kwa masaa.
Kwa sababu sehemu kubwa ya kazi zilikuwa za mikono na mtu alikuwa na jukumu moja na linalopimika, kadiri mtu alivyoweka masaa zaidi kwenye kazi, ndivyo alivyozalisha zaidi.
Tumeshaondoka kwenye zama za viwanda na sasa tuko kwenye zama za taarifa, kazi nyingi kwa sasa zinahusisha taarifa na maarifa kuliko mikono. Lakini bado kazi zimekuwa zinapimwa kwa masaa.
Tabia hii ya kupima kazi kwa masaa ambayo mtu amekuwa kazini, siyo tu haipimi kazi sawasawa, bali pia inapunguza ufanisi wa kazi. Hiyo ni kwa sababu kadiri mtu anavyoweka masaa mengi kwenye kazi, ndivyo akili yake inachoka na kujikuta anafanya kazi isiyo na viwango vizuri.
Mpaka sasa wastani wa kufanya kazi kwa siku ni angalau masaa nane, kitu ambacho tumetoka nacho kwenye zama za viwanda. Lakini kwa kazi yoyote inayohusisha maarifa, yaani ambayo unatumia akili yako kufikiri, kufanya maamuzi na kuja na ubunifu, akili hiyo haiwezi kufanya kazi mfululizo kwa masaa nane.
Huna masaa nane ya kufanya kazi ya kufikiri na ubunifu, kwa kiwango cha juu kabisa unaweza kufanya hivyo kwa masaa yasiyozidi matatu, wengi kiwango cha juu ni masaa mawili. Baada ya hapo akili inakuwa imechoka na haiwezi tena kuwa na ufanisi wa hali ya juu.
Kwa ujumbe huu wa leo, kuna mambo muhimu sana tunapaswa kuondoka nayo hapa kuhusu mafanikio.
Moja ni kulinda muda wa kuweka kazi hasa, kwa kuwa tunajua hakuna mafanikio bila kazi, na kwa kuwa tunajua kazi nyingi zinahitaji akili zetu kuwa na nguvu ya kufikiri na ubunifu, tunapaswa kutenga muda wa kukamilisha yale majukumu yetu muhimu. Tujue kipi kinahitaji umakini wetu zaidi na kukipa umakini huo kabla ya mambo mengine.
Mbili ni kujikinga na kila aina ya usumbufu, kwa sasa mtaji mkubwa ulionao kwenye chochote unachofanya ni umakini wako, lakini pia umakini huo unawindwa na watu wengi. Kuanzia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, na wengine wanaotaka kuwasiliana na wewe kwa namna moja au nyingine. Akili yako inapokuwa kwenye usumbufu, haiwezi kuweka umakini kwenye kazi unayofanya. Kwa kuwa kiwango cha juu cha akili kuwa kwenye umakini ni kifupi, ondoa kabisa usumbufu kwenye kipindi hicho. Kama ni simu kaa nayo mbali na kama ni eneo basi kuwa sehemu tulivu ambayo hakuna usumbufu.
Tatu ni pima ufanisi wako kwa matokeo unayozalisha na siyo kwa muda uliotumia kufanya kazi. Unapata kile unachopima, ukipima ni masaa mangapi unafanya kazi, utajikuta unaweka masaa mengi zaidi lakini hakuna unachozalisha. Ukianza kupima matokeo unayozalisha, utajisukuma kuzalisha matokeo zaidi. Panga ni wapi unataka kufika au nini unataka kufikia kisha tenga muda wa kuweka juhudi, jipime kwa matokeo unayozalisha na siyo muda ulioweka kwenye kazi hiyo.
Kazi zetu nyingi kwa sasa zinahusisha zaidi maarifa kuliko mikono, zingatia haya ili uweze kutumia vizuru umakini wako kuzalisha matokeo yatakayokutofautisha na wengine na kukuwezesha kufanya makubwa.
Kama ukiweza kutenga masaa mawili tu kila siku, ambayo unaweka kazi kwa umakini mkubwa bila kuruhusu usumbufu wowote, yaani dakika zote 120 unazipeleka kwenye kile unachofanya, ndani ya miaka mitano utakuwa umepiga hatua kubwa kuliko wengine wote wanaofanya kazi kama yako lakini hawapati wakati wa umakini kama wako. Lipe hili umakini na utakuja kuvuna matunda yake baadaye.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Asante sana,huu ukurasa maalumu kwa sisi watumishi
Si muda uliokaa kazini bali ni matokeo gani umepata kwa kuwa kazini.
Ukiwa na picha ya matokeo unayotaka kupata kwenye kazi yako wala hutaumizwa na wanaochelewa kazini(college)au anaekutegea kazi maana wao wamefungwa kwa muda wewe ni matokeo.Tukielewa dhana hii huhitaji kusimamiwa na mtu kwa kazi zako.
LikeLike
Kabisa Hendry,
Ukiacha kuangalia muda na ukaangalia matokeo unayozalisha, unapiga hatua kubwa.
LikeLike