Kila mtu huwa ana uimara na madhaifu yake.
Lakini madhaifu tuliyonayo yanaweza kugawanyika katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni madhaifu ya kweli, yale ambayo mtu umezaliwa nayo na ni vigumu kuyabadili. Mfano kama wewe ni mfupi sana na unataka kucheza mpira wa kikapu, huwezi kujibadili na kuwa mrefu, hivyo huo ni udhaifu ambao utakuwa kikwazo kwenye hilo. Madhaifu ya kweli huna namna ya kuyabadili na ukikazana kuyabadili unaishia kuwa hovyo zaidi, kwa sababu unaondoa nguvu kwenye uimara wako na kujirudisha nyuma.
Sehemu ya pili ni madhaifu uchwara, haya ni madhaifu ambayo siyo ya kuzaliwa nayo na wala siyo ya kweli kutoka ndani yako. Ni madhaifu ambayo mtu unakuwa umejifunza kwenye mazingira, jamii au kutokana na mazoea ambayo mtu anakuwa amejijengea. Haya ni madhaifu ambayo mtu unaweza kuyabadili na yakaacha kuwa kikwazo kwako kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
Hapa nakushirikisha baadhi ya madhaifu uchwara, ambayo wengi tunayo na yamekuwa kikwazo kwetu kupiga hatua.
- Tabia ya kupenda kila mtu akubaliane na wewe na kuona wale wasiokubaliana na wewe ni maadui kwako. Huu ni udhaifu unaokunyima fursa ya kushirikiana na watu wazuri ambao wanafikiri na kuamini tofauti na wewe. Kuondokana na udhaifu huu kubali siyo kila mtu anakubaliana na wewe, hivyo shirikiana nao kwa kile mnachoweza kufanya pamoja.
- Tabia ya kutaka kuwabadili watu wengine na wawe kama unavyotaka wewe. Udhaifu huu unakuchosha kwa sababu watu huwa hawapendwi kubadilishwa. Kuondokana na udhaifu huu chagua watu ambao unaweza kwenda nao kama walivyo na siyo kuchukua mtu na kujiambia utambadili, utapoteza nguvu zako bure.
- Tabia ya kupenda kujali watu wengine wanafikiria nini kuhusu wewe au wanakuchukuliaje. Udhaifu huu unakufanya uishi maisha ya maigizo, ili watu wakuone kwa namna fulani na kukuchukulia hivyo. Tambua hakuna anayekufikiria kama unavyofikiri, kila mtu anapambana na hali yake hivyo chagua kuyaishi maisha yako kwa namna unavyotaka wewe.
- Tabia ya kufuata mkumbo, kwa kuwa wengi wanafanya kitu basi unaona ndiyo sahihi kufanya. Tambua kitu hakiwi sahihi kwa sababu wengi wanakifanya, jua usahihi wa kitu kabla hujaingia kufanya, kama siyo sahihi, hata kama kila mtu anafanya, usifanye.
- Tabia ya kupenda makubwa bila ya kulipa gharama inayohusika, huu ni udhaifu ambao umewaingiza wengi kwenye utapeli. Unaambiwa kuna njia ya mafanikio ya haraka bila ya kuweka kazi, unaikimbilia na kuishia kupoteza muda na fedha. Tambua hakuna njia ya mkato ya mafanikio, mafanikio ya kweli yameambatana na gharama ambayo lazima mtu uilipe, kama unaambiwa kuna mafanikio bila kulipa gharama, kimbia haraka sana, unakwenda kutapeliwa.
Haya ni madhaifu ambayo wengi wanayo na yanawakwamisha, ukiweza kuondokana nayo, utakuwa umeondoa kikwazo kikubwa kwenye mafanikio yako. Uzuri ni iko ndani ya uwezo wako kuondokana na madhaifu yote haya.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Ahsante Sana kocha
LikeLike
Karibu.
LikeLike
Asante sana Kocha kwa madhaifu haya Uchwara.
Tabia namba nne ni kitu ambacho kimepotea ndoto za wengi sanaa, Wengi tumethiriwa na dhana ya wengi wape au wengi wapo sahihi, wengi wamekuwa na hofu kutokana na dhana potofu kuwa akionekana na misimamo ya peke yake ataonekana wa ajabu au “mchawi” kumbe ndio kujipoteza zaidi.
LikeLike
Kabisa Mahule,
Kutaka kupendwa na kukubalika na wengine, imekuwa kikwazo kwa wengi kupiga hatua.
LikeLike
Madhaifu haya ni kweli yametuangusha wengi, na hata kusema kwamba tunayafanyia kazi kama ilishakuwa tabia kuivunja inachukuwa muda mrefu. Asante kocha na uwe na siku njema.
LikeLike
Karibu Kalenga.
LikeLike
Nitayaepuka madhaifu uchwara ili niweze kuwa na maisha ya utulivu na kujiamini.
Shukrani sana kocha kwa makala hii.
LikeLike
Vizuri Datius.
LikeLike