Mwandishi mmoja amewahi kusema kadiri mtu unavyolazimisha kwamba maamuzi yako hayaathiriwi na hisia ndivyo maamuzi hayo yanavyokuwa na hisia.
Wote tunajua kwamba sisi binadamu ni viumbe wa kihisia, maamuzi mengi tunayofanya ni kwa hisia kwanza na baadaye tunayahalalisha kwa kufikiri. Lakini tunapenda kujiaminisha kwamba tunafanya maamuzi yetu kwa kufikiri, kitu ambacho siyo kweli.
Linaloambatana na hisia, ni ushawishi wa wengine kwenye maamuzi mengi tunayofanya.
Maamuzi mengi unayofanya kwenye maisha yako, siyo kwa mapenzi yako binafsi, bali kwa ushawishi wa watu wengine.
Na kwa zama tunazoishi sasa, zama za usumbufu wa kila aina, karibu kila tunachofanya ni kwa sababu wengine wanafanya au tunataka kuwaonesha wengine kwamba na sisi tunafanya.
Tukianza na matangazo ya bidhaa mbalimbali, makampuni yote makubwa huwa yanaendesha matangazo yasiyo na ukomo, yote ni kuhakikisha kwamba kila wakati unafikiria kuhusu bidhaa na huduma za makampuni hayo. Unapoona ujumbe ule ule kila wakati, unaathiri sana maamuzi unayokwenda kufanya.
Kitu kingine kinachoathiri maamuzi yetu ni propaganda mbalimbali ambazo zimekuwa zinaendeshwa na serikali, wanasiasa, dini na taasisi nyingine ili kuathiri fikra za watu na kuwasukuma kufanya maamuzi fulani.
Funga kazi iko kwenye mitandao ya kijamii, hii ndiyo inaathiri karibu kila kitu tunachofikiria na kufanya. Kila anayeshiriki kwenye mitandao ya kijamii anaathiriwa na kuwaathiri wengine bila hata ya kujua kinachoendelea.
Chukua mfano umemuona mtu amevaa nguo ya aina fulani, au ameenda matembezi eneo fulani, au ana gari ya aina fulani. Moja kwa moja na wewe unafikiria kuwa na vitu hivyo ambavyo wengine wanavyo. Unaweza kujiambia unavihitaji sana, unaweza kuhalalisha utakavyo, lakini tambua kwamba hayakuwa maamuzi yako toka awali, uliona wengine wakiwa navyo.
Kwa kutambua namna maamuzi yetu yanavyoathiriwa na wengine, tunaweza kutumia kwa njia mbili.
Moja ni kuacha kujidanganya na kutambua ushawishi ulio nyuma ya kila maamuzi tunayofanya. Huwezi kuepuka ushawishi kabisa, lakini ni vizuri kujua ni kipi kimekusukuma wewe kufikia maamuzi fulani. Hivyo kupima kama maamuzi hayo yana manufaa kwako au la. Kila maamuzi unayofanya, jiulize ushawishi umetoka wapi, jiulize ni wakati gani ulipata wazo hilo na ulilipata katika mazingira gani. Kisha pima manufaa kabla hujaendelea. Usikubali msukumo wa wengine ukuingize kwenye maamuzi yanayokugharimu.
Mbili ni kutumia ushawishi wa kichini chini kuwafikia walengwa wa kile unachofanya. Kwa kazi au biashara unayofanya, jua wale unaowalenga na tengeneza namna ya kuwafanya wawe wanakufikiria muda wote. Inaweza kuwa mawasiliano nao ya mara kwa mara hasa kwa njia ya ujumbe au kuwa na njia nyingine inayowafanya wale unaowalenga wakufikirie kwa namna nzuri. Na pale wanapokuwa na uhitaji wa kile unachofanya, mtu wa kwanza kufikiriwa ni wewe.
Sehemu kubwa kama siyo yote ya maamuzi tunayofanya huwa yanaathiriwa na wengine, tambua hili ili kuhakikisha unafanya maamuzi yenye manufaa kwako.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,