“Inaction breeds doubt and fear. Action breeds confidence and courage. If you want to conquer fear, do not sit home and think about it. Go out and get busy.” — Dale Carnegie

Kila unapopanga kufanya kitu chochote kipya na kikubwa, hofu inakuingia.
Unapata hofu hiyo siyo kwa sababu huwezi, bali kwa kuwa ni kitu ambacho hujazoea kufanya.
Ni kawaida kwa binadamu kujawa na hofu pale anapokabiliana na kitu chochote kipya.

Hofu imekuwa kikwazo kwa wengi kwa sababu wanakabiliana nayo kwa namna isiyo sahihi.
Wengi wanapopatwa na hofu huacha kufanya, kwa kujiambia bado hawajawa tayari.
Lakini hilo limekuwa halisaidii, kwani wanapoacha kufanya, ndiyo hofu inazidi kuwa kubwa.

Kutokuchukua hatua hua kunazalisha wasiwasi na hofu.
Kuchukua hatua huwa kunazalisha ujasiri na kujiamini.
Hivyo kama unataka kuishinda hofu, usiache kuchukua hatua na kuifikiria, badala yake anza kuchukua hatua.
Hata kama unajiona hujawa tayari, wewe anza kuchukua hatua.
Unapoanza kufanya, unaona kumbe mambo siyo makubwa na magumu kama ulivyokuwa unayachukulia.

Dawa kuu ya hofu ni kufanya kile unachohofia.
Inakujengea kujiamini na ujasiri na kukusukuma kuendelea zaidi.
Kwa chochote unachohofia kufanya, anza kukifanya.
Usijiambie hujawa tayari, usijiambie unajipanga zaidi.
Wewe anza kufanya na utaona kumbe mambo siyo magumu kama ulivyokuwa unachukulia awali.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu mambo ambayo hupaswi kutumia nguvu, yasome hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/08/2139

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.