“It’s easy to be great. It’s hard to be consistent.” – Steve Martin
Kuna watu wengi ambao huwa wanafanikiwa kupiga hatua fulani, lakini baada ya hapo wanaanguka vibaya.
Kufanikiwa siyo kitu kigumu sana, ila kubaki kwenye mafanikio hayo ndiyo kitu kigumu na kinachowashinda wengi.
Kubaki kwenye mafanikio inamtaka mtu kuwa na msimamo wa hali ya juu,
Kuendelea kufanya kile kilichomfikisha kwenye mafanikio hayo, huku akiboresha bila ya kuchoka.
Tatizo letu kubwa ni huwa tunachoka na kuzoea vitu haraka.
Unaweza kupata msukumo mkubwa wa kufanya mazoezi makali kwa siku chache, lakini baadaye unarudi kwenye mazoea.
Unaweza kukutana na fursa fulani ukasukumwa kuifanyia kazi kubwa kwa siku chache, lakini baada ya hapo ukarudi kwenye mazoea.
Kama mafanikio ya kudumu yangekuwa yanapatikana kwa mtu kufanya kitu mara moja, kila mtu angekuwa amefanikiwa sana.
Lakini sivyo mafanikio yalivyo, ukifanya mara moja unaweza kupata matokeo makubwa, lakini ni msimamo wa kuendelea kufanya ndiyo utakuweka kwenye mafanikio hayo.
Kinachowazuia wengi wasiwe na msinamo wa kuendelea kufanya ni kwa sababu ya uchovu na kuboreka.
Mwanzo mtu anakuwa na hamasa na kuweza kujituma kufanya kwa sababu ya upya wa kitu.
Baada ya muda mtu anachoka na kuzoea na hapo msukumo na hamasa vinaisha.
Ndiyo maana wengi wasiojua msingi huu, huwa wanakimbizana na fursa mpya kila wakati, wanajidanganya kwamba fursa hizo mpya ni nzuri kuliko wanachofanya sasa, lakini ukweli ni wamekosa msimamo wa kuendelea kufanya kile ambacho walishaanza.
Jijengee msimamo, unapopanga kufanya kitu, hakikisha utaendelea kukifanya, hata ukishafanikiwa.
Hiyo ndiyo njia pekee ya kubali kwenye mafanikio makubwa.
Kila wakati jikumbushe kuwa na msimamo, hapo ndipo mafanikio yako makubwa yalipo.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu jinsi unavyoshawishiwa kufanya maamuzi yanayokugharimu, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/09/2140
Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.