“Each of us is born with a box of matches inside us but we can’t strike them all by ourselves.”
— Laura Esquivel

Njiti ya kibeririti ina uwezo mkubwa wa kuanzisha moto, lakini haiwezi kuanzisha moto huo yenyewe.
Ni lazima isubuliwe na kitu kingine ndiyo iweze kuanzisha moto.
Chuma pia hufuliwa kabla haijaweza kutumika kwa manufaa.
Dhahabu husafishwa kabla haijatengeneza vito vya thamani.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwetu wanadamu.
Ndani yako una uwezo mkubwa, unaweza kufanya makubwa sana, lakini hutaweza kuyafanya peke yako.
Hutaweza kufikia makubwa kwa kubaki kwenye mazoea.
Ni lazima usuguliwe, lazima ufuliwe, lazima usafishwe.

Utaweza kufikia uwezo mkubwa ulio ndani yako kwa kukutana na wengine wanaokusukuma kufikia uwezo huo, kwa kukutana na changamoto mbalimbali na kwa kuwa tayari kujifunza na kubadilika, kuwa bora zaidi.
Kama hutakuwa tayari kwa haya, uwezo mkubwa ulio ndani yako utapotea bure.

Asubuhi ya leo tafakari ni kwa kiasi gani unapambana ili kufikia uwezo wako mkubwa.
Kwa kiasi gani unazungukwa na watu wanaokusukuma ufanye makubwa zaidi.
Kwa kiasi gani unajifunza na kuchukua hatua kwa yale unayojifunza.
Kama huchukui hatua hizi, kama kila siku unabaki kwenye mazoea, jua unapoteza uwezo mkubwa ulio ndani yako.

Huwezi kuwa bora bila kufuliwa, hivyo jiweke kwenye mazingira yanayokufua na kukufanya kuwa bora zaidi.

#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu siyo wewe peke yako, soma zaidi hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/13/2144

Rafiki yako,
Kocha Dr Makirita Amani.