Nguvu, muda na pesa ni rasilimali muhimu sana kwenye safari ya mafanikio.

Muda tumekuwa tunauzungumzia sana, jinsi ambavyo unapaswa kutumia fedha kuokoa muda badala ya kutumia muda kuokoa fedha. Tumejifunza sana kuhusu ukomo wa muda, kwamba ukishapotea haurudi tena, hivyo tunapaswa kuwa na ubahili nao kuliko tunavyokuwa na ubahili na fedha.

Pesa unazijua mwenyewe, ukiwa na pesa kidogo unazipangilia kwa kuzingatia vipaumbele vyako, hukubali kupoteza pesa pale ambapo una uhitaji mkubwa wa fedha. Lakini wengi bado wana changamoto kwenye pesa nyingi, pale wanapopata pesa nyingi wamekuwa wanavurugwa na kushindwa kutulia, wanajikuta wakizitumia hovyo na kuzipoteza.

Changamoto kubwa ipo kwenye nguvu na hapa nazungumzia nguvu za mwili. Hii ni rasilimali ambayo wengi wamekuwa hawaipi uzito unaostahili.

Nimekuwa napenda kuchukulia mfano wa betri ya simu, kwa sababu kila mtu ana simu hivyo ni rahisi kuelewa. Kama usiku umeweka simu yako kwenye chaji na kuamka asubuhi ikakuambia imejaa kwa asilimia 100, unajua kila unachofanya kwenye simu kinapunguza chaji. Ukiingia mtandaoni na kufungua vitu vingine kwenye simu, chaji inapungua. Ilikuwa asilimia 100, mara unashangaa asilimia 98, mara asilimia 90 na kuendelea.

Kama kuna siku unajua utakwenda mbali na hutaweza kuchaji tena simu yako, unakuwa mwangalifu, yale yasiyo muhimu kwenye simu huyafanyi, kwa sababu hutaki chaji ya simu yako ipotee.

Hivyo ndivyo mwili wako ulivyo. Unapolala usiku ndiyo unauchaji, hivyo ukiamka asubuhi mwili unakuwa na nguvu za kutosha. Lakini kila unachofanya kinapunguza nguvu za mwili wako. Chochote kile unachofanya, hata kiwe kidogo kiasi gani, kinatumia nguvu ya mwili. Sasa kwa kuwa nguvu za mwili wako zina ukomo, kadiri unavyozitumia ndivyo zinavyoisha na inakuwa vigumu kwako kufanya mambo muhimu.

Ndiyo maana huwa ni rahisi kufanya majukumu magumu mapema kwenye siku yako kuliko siku inapokuwa inaisha, kwa sababu mapema bado unakuwa na nguvu lakini kadiri siku inavyoisha nguvu hizo zinapungua.

Sasa kikwazo kwa wengi kufanya makubwa na kuweza kufanikiwa, ni kutawanya nguvu za mwili kwenye mambo yasiyo muhimu.

Kuna mambo watu wamekuwa wanafanya kwa mazoea, lakini mambo hayo yanatumia nguvu nyingi za mwili na kumuacha mtu akiwa amechoka na asiweze kuchukua hatua sahihi.

Fikra na hisia hasi huwa zinanyonya nguvu kubwa ya mwili na kumuacha mtu akiwa amechoka na asiweze kufanya yale muhimu. Epuka sana fikra na hisia hizo hasi, ambazo ni hofu, hasira, wivu, chuki na nyinginezo.

Kufuatilia habari na mitandao ya kijamii ni kitu kingine ambacho kinanyonya sana nguvu za mwili na kumchosha mtu kiasi cha kushindwa kufanya yale muhimu.

Ulaji na unywaji usio sahihi pia umekuwa unachosha sana mwili. Vyakula vya wanga na sukari kwa wingi, vilevi na vinywaji vinavyochangamsha huwa vinauacha mwili ukiwa umechoka zaidi.

Kuwa makini sana na nguvu za mwili wako, kila unapoamka pata picha ni betri la mwili wako liko kwenye asilimia 100 na huwezi kulichaji tena katikati ya siku, ni mpaka siku hiyo iishe. Ukishapata picha hii, jiulize utatumiaje chaji ya betri ya mwili wako ili inapoisha uwe umefanya mambo yenye tija.

Anza kwa kutenga masaa mawili ya mwanzo ya siku yako kutekeleza majukumu muhimu yanayohitaji umakini wako mkubwa. Hapo hakikisha unakuwa kwenye utulivu mkubwa na hakuna usumbufu wowote unaochukua nguvu zako. Katika muda huo, usifanye chochote ambacho kinanyonya nguvu za mwili wako, peleka umakini wako wote kwenye jukumu moja muhimu sana, ambalo ukilikamilisha siku yako itakuwa yenye manufaa.

Kuwa makini na nguvu za mwili wako unazozitawanya hovyo, kwa chochote unachokipa umakini wako, kuanzia kwenye fikra, hisia na hatua unazochukua, jiulize kama ndiyo kitu muhimu na kinachokufikisha kule unakotaka kwenda, kama siyo basi achana nacho mara moja. Peleka nguvu yako kwenye mambo yenye mchango wa kule unakotaka kufika.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha