Safari ya mafanikio, kama ambavyo nimekuwa nakushirikisha mara kwa mara, ni ya muda mrefu, inahitaji msimamo na uvumilivu mkubwa.

Hali hiyo inakaribisha uchovu, kwa sababu siyo kawaida kwetu binadamu kufanya kitu kwa muda mrefu, hasa pale unapohitajika kukazana kuwa bora kila wakati.

Tumekuwa tunashirikishana njia nyingi za kukabiliana na uchovu huo, ikiwepo kupangilia vizuri matumizi ya muda na nguvu zako.

Ipo njia nyingine nzuri unayoweza kuitumia kukabiliana na uchovu, ukaweza kujisukuma hata pale unapokuwa huna hamasa ndani yako.

Njia hiyo ni kufanya kama unatoa zawadi kwa mtu ambaye ana uhitaji mkubwa sana.

Chochote kile unachotaka kufanya lakini unaona umechoka au huna hamasa, kichukulie ni zawadi unayompa yule anayenufaika nacho, akiwa kwenye uhitaji mkubwa wa kile unachofanya.

Kama ni uandishi, ona kile unachoandika kama zawadi kwa mtu ambaye amekwama kwenye hali fulani, ambapo kupitia unachoandika anaweza kujikwamua.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye kazi yoyote ambayo mtu unafanya, iwe unafundisha, unatibu, unaongoza au chochote kile, ona kile unachofanya kama zawadi kwa wale wanaokitegemea, kwa sababu bila ya wewe kukamilisha wajibu wako kuna namna watakwama.

Kadhalika kwenye biashara, chukulia kile unachouza kama zawadi unayoitoa kwa wale wenye uhitaji. Japokuwa wanakulipa kukipata, lakini bado wasingeweza kutatua mahitaji yao kama wewe usingekuwepo, licha ya kuwa na fedha. Hivyo unawapa zawadi ya wao kuweza kutatua changamoto zao au kukamilisha mahitaji yao.

Kwa kuchukulia kile unachotoa kama zawadi unapata msukumo wa aina mbili. Moja ni msukumo wa kusaidia wale ambao wanakwama bila uwepo wako. Na mbili ni majuto ambayo utakuwa nayo kwa kuona umeshindwa kumsaidia mtu kitu ambacho kilikuwa ndani ya uwezo wako. Nguvu hizo mbili zinakupa hamasa ya kuendelea pale unapojiona umechoka au unataka kukata tamaa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha