
Utangulizi
Mwandishi anaanza na kusema kuwa ili ufanikiwe katika kukuza mtandao wa mafanikio wa watu basi ni muhimu mtu kuvuka kikwazo cha hofu au aibu katika kukutana na watu wapya au mtandao wa watu wageni kwako. Umuhimu wa kukutana na watu wapya una faida kede kede katika upatikanaji wa fursa za kazi, ukuaji wa biashara na kupata mawazo mapya yanayoweza kubadilisha maisha ya mtu.
Kitabu hiki mwandishi anatoa ushauri na miongozo ya namna kuhusiana na watu katika jamii au eneo la kazi katika kukuza uwanja mpana wa kukutana na watu wapya unaosaidia watu kukua kibiashara. Huenda kukutana kwa watu wapya kukufanyika ana kwa ana au hata njia ya mtandao kwa wakati huu tuishio. Kitabu hiki hivyo ni muhimu kwa kila mtu mwenye kutaka kukua kikazi, kielimu na kibiashara katika upya wa kukutana na watu na mawazo mapya.
Wakati huu tuishio unazo fursa nyingi za mtu kukutana na watu wapya kila siku. Hii ipo maeneo yote kuanzia maeneo ya kazi, ofisini, shuleni, vyuoni, makongamano na hata mitandaoni. Kwa mtu ambaye ana ujuzi wa kuhusiana na watu vizuri basi ana nafasi kubwa ya kufanikiwa kuwa na mtandao mkubwa wa watu wa mafanikio. Watu ni mtaji na wanasema kinachotafutwa maishani kikubwa katika mapambano ya mafanikio ni pamoja na nani anayekujua.
Mwandishi anasema juu ya mambo makubwa manne yanayomsaidia mtu kuwa mtu aliyefanikiwa katika kukuza mtandao wa kuwa na watu wapya kila siku. Mambo haya manne ukiyaangalia unaona ni kweli yanapatikana katika watu ambao wamefanikiwa kuwa na mtandao mkubwa wa watu.
Mosi, “Udadisi”. Watu wengi wenye udadisi wana nafasi kubwa ya kuwa na watu wengi katika mtandao wao. Udadisi au uulizaji maswali katika mazungumzo unasaidia kufungua fursa ambazo mtu asingesema bila kuulizwa. Uwe na udadisi itakusaidia kukutana na watu wengi wapya.
Pili, “Ukarimu”. Watu wengi wanaofikika au wenye kukarimu watu basi watu wengi wanapenda kuwa nao karibu. Hili linampa mtu nafasi ya kukuza mtandao wa watu na watu ndio mtaji wa mambo mengi tutafutayo maishani.
Tatu, “Ujasiri”. Watu walio na ujasiri ni watu wenye uthubutu na hili linawasaidia sana kutohofu kuzungumza na watu mbalimbali iwe watu wa chini, watu maarufu, viongozi na kadhalika. Inasaidia sana kuwa na watu wengi ambao watavutika kwa mtu huyo sababu ya mtu kuwa jasiri.
Nne, “Hamasa”. Watu wengi ambao wanawapa hamasa watu wengine kufanya kitu fulani. Huwa na nafasi kubwa ya kuwa na watu wapya wengi sana. Hili liko wazi kwa kuona wazungumzaji, wanenaji, walimu au wachambuzi wa mambo kuwa na watu wengi wanaowatafuta na kutaka kuzungumza nao. Hili hugeuka kuwa na nafasi nzuri ya mtu kukutana na fursa mpya kutoka kwa watu wapya.
Haya mambo manne yanapokuwa kwa pamoja ndani ya mtu ndio yanayomsaidia awe na nafasi nzuri ya kukutana na watu wapya kila siku na inampa kumfungulia milango ya fursa za ajira, wengine “Connections”, mawazo mapya na fursa nyingine nzuri nzuri za kibiashara.
Safari ndani ya Sura za Kitabu
Nimependa kuongeza hiki kitu katika uchambuzi wa kitabu kwa kusafiri katika sura na kuchagua mambo mbalimbali muhimu na ya mchango kwa mtu akibeba na kufanyia kazi.
Kipengele hiki kinakuwa mchanganyiko katika kuchukua baadhi ya vifungu vya sentensi zenye kubeba maarifa fulani makubwa yenye mchango na matokeo makubwa.
Hiki kipengele nitajaribu au nitakuwa naweka angalau mambo kama 29 hadi 30 ambayo ndani ya safari ya sura za kitabu nimeyapata. Naamini itarahisisha kujua kwa sehemu au asimilia 50% nini kitabu kimebeba kwa ajili ya kueleza jambo.
1. Suala la kukuza mtandao wa watu wa mafanikio si pekee kushughulika na watu wapya ambao huwajawajua bali hata watu wako wa karibu ni muhimu kutambua bado ni sehemu ya mtandao mkubwa wa mafanikio. Usisahau familia yako, marafiki zako, watu mlosoma pamoja shuleni au chuoni na watu wa jamii inayokuzunguka. Kundi hili nalo bado linakua na lina hazina ya fursa mpya zimefichwa. Hujui ndugu yako au rafiki yako anahusiana na nani au anamfahamu nani.
2. Unapoweza kukua vizuri na kukomaa katika kuwa na mtandao mkubwa wa watu inakusaidia sana katika kupata uwanja mpana wa watu wanaoweza kukusaidia katika jambo unaloweza kukutana nao. Uwepo wao unaweza kurahisisha sana kupatikana kwa majibu ya mambo yanayoweza kukusumbua.
3. Kadri unavyoweza kuwa na nambari nyingi za watu au mawasiliano ya watu iwe ni nambari za simu, barua pepe ndivyo ilivyo nafasi kubwa ya kujitengenezea fursa za ajira, biashara na mawazo mapya. Katika orodha yako ya watu ulowahifadhi basi ndipo ilipo hazina kubwa ya watu wengi ambao kwa mahusiano mazuri utakayojenga yatakusaidia kupiga hatua kubwa maishani.
4. Kabla hujaanza kutafuta mtandao mpya wa watu. Ni muhimu sana utambue nini thamani ambayo na wewe utakayokuwa tayari kutoa kwao. Mahusiano mazuri ya kibiashara huanza katika namna pande zote mbili zinavyofaidika na uwepo wa hao watu wawili. Kiufupi “thamani”. Tengeneza mtandao na watu wapya kwa lengo kubwa kuanzisha mahusiano mapya ya kibiashara zaidi kuliko makusudio mengine.
5. Mahusiano ya kibiashara yanajengwa katika muda. Huwezi kupata leo mtu mpya katika mtandao wako wa watu na ukaanza kukopa au kujieleza vitu vya ndani kabla hujamjua mtu huyo kwa undani. Hili ni kosa kubwa ambalo watu wengi wanapokutana na watu wapya wanasahau kuwa mahusiano ya watu hadi kufikia yakawa mahusiano yanafungua fursa za kazi au biashara hutaka kwanza muda wa kuyakuza. Ukikuza mahusiano ya kibiashara vizuri sasa basi baadaye huleta matokeo mazuri mno.
6. Carl Jung anasema “The Meeting of Two Personalities is like the contact of two chemical substances: If there is any reaction, both are transformed”. Hii ikiwa na maana kubwa kuwa “Makutaniko ya watu wawili wa haiba zinazolingana ni sawa na kemikali mbili ziunganikapo huleta badiliko la tofauti au mapinduzi. Hili lipo katika kutafuta mtandao sahihi wa watu. Unapokutana na mtu au watu wenye haiba zinazolingana basi usipoteze hiyo nafasi katika kuitumia. Ni bahati mno ukipata watu mnaofanana na kuwa na mwelekeo mmoja katika maisha.
7. Ikiwa ni kampuni basi ujenzi wa watu wapya au mtandao mpya wa watu unaweza kuwa katika ngazi kubwa mbili. Mosi, ngazi ya ndani ya kampuni kwa maana ya wasimamizi wakuu wa kampuni, wafanyakazi na wasaidizi wa wafanyakazi. Pili, ngazi ya nje na kampuni ambao ni wateja, wasambazaji na washindani.
8. Mawazo mapya ya kibiashara yanaweza kuchochewa na wafanyabiashara kuwa na makutano ya kibiashara yanayoweza kufanyika kila mwezi au kwa mwaka mara moja. Matukano haya yanapokuwa na lengo la kukua zaidi basi yahusishe watu wa biashara tofauti, wataaluma na wakati mwingine watu wa sekta ya viwanda. Makutano haya yanaweza kufanywa asubuhi, mchana au chakula cha jioni katika eneo tulivu.
9. Kuna makutano mengine ya wafanyabiashara ambayo huwa na lengo la kubadilishana mawasiliano ya wateja au wateja watarajiwa. Makutano haya humsaidia kila mshiriki kupata mapendekezo ya wateja (referrals) ambapo mtu anapewa mtandao wa wateja wapya ashughulike nao.
10. Kabla hujaenda katika tukio lolote ambalo unajua litahusisha watu wengi basi kuna mambo muhimu ya kuzingatia. Mosi, jua aina ya watu ambao watakuwepo katika tukio hii itakusaidia kujipanga kimwonekano na hata uulizaji wa maswali au aina ya mazungumzo. Pili jiandae kuwa mtu chanya unapoenda katika tukio lolote lile . Tatu, ni suala la mwonekano kimavazi, mavazi yanasema zaidi kabla ya kuanza kumjua mtu.
11. Lengo mojawapo mama la uwepo wa interneti ni taarifa. Ni sawa tu na makutano ya watu ana kwa ana bado yanakaa katika lengo la mazungumzo ya taarifa. Hivyo kwa kukuza mtandao mzuri wa watu mtandaoni ni muhimu kushirikisha taarifa bora zenye kutoa thamani na kuvuta watu unaotaka wawe katika mzunguko wa watu unaotaka kukua nao kibiashara au kikazi.
12. Matumizi ya barua pepe yameshuka kidogo kwa watu wengi mara baada ya majukwaa ya mtandaoni kuwepo. Ila haitoi ukweli kuwa matumizi ya barua pepe bado yana umuhimu mkubwa katika kukuza mtandao sahihi wa watu, kutumiwa kwa kazi za kiofisi, uandishi, biashara na makampuni pamoja na mtu mmoja mmoja.
13. Majukwaa ya jamii “Forums”. Ni njia nyingine nzuri sana ya kukutana na watu wapya na wakabadilishana uzoefu, usambaaji wa taarifa na kukutana na fursa. Yapo hayo majukwaa mengi katika interneti kulingana na kile unachokihitaji. Majukwaa mengine ni pamoja na “Facebook na Twitter”.
14. Ni jambo zuri kuwa na mtandao mpya wa watu kupitia njia mbalimbali iwe kwa ana kwa ana au mtandaoni. Ila kuna vitu vya kuchukua tahadhari unapokutana na watu wapya kutokuwa mtu mwepesi kutoa haki yako ya usiri na uwazi. Watu wengi huamini watu haraka ambao ni wapya pasipo kujua lolote laweza kutokea.
15. Stuart Henderson Britt anasema “Doing Business without advertising is like winking at a girl in the dark. You know what you are doing, but nobody else does”. Ikiwa na maana Unapofanya biashara na hauitangazi biashara yako ni sawa na kukonyeza msichana katika chumba chenye kiza. Wewe utakuwa unajua unachokifanya ila watu hawatajua hilo. Biashara yako unaitangazaje ?. Wakati huu tuishio unaweza kuwa na kadi ya biashara, vipeperushi, mabango, stika na matangazo kwa njia ya redio, magazeti au televisheni. Tangaza biashara yako watu wajue unauza nini.
16. Kadi yako ya biashara iwe na taarifa muhimu kuhusu biashara yako. Weka mawasiliano yanayopatikana, huduma unazotoa au bidhaa unazouza na weka mahali unapopatikana. Kadi ya biashara “Business cards” ni utambulisho mfupi wa biashara yako kwa maneno machache.
17. Mwonekano wa siku ya kwanza katika makutano ya watu una nafasi kubwa katika kukuza mtandao wa watu wapya. Mwonekano nadhifu ni muhimu mno.
18. Unapokuwa katika mazungumzo na watu iwe ni tukio au eneo la kukutanisha watu wengi basi ijue sanaa ya mazungumzo (Art of Conservation). Mazungumzo huhusisha kuongea na kusikiliza. Kusikiliza ni muhimu sana katika mazungumzo pengine hata kuongea. Kuwa msikilizaji mzuri unapokuwa na mazungumzo na watu. Hili litakupa nafasi kubwa ya kuvutiwa na watu wengi.
19. Katika kukutana na watu wapya na kutamani kukuza mahusiano na watu wapya. Inaweza kutokea umezuiliwa na mtu (Blocked) au kuondolewa katika kundi pengine kwa kosa la namna ulivyofanya kitu (Approaching Problems). Ila ukibadilisha na kujifunza namna ya kuishi na watu wapya unaweza kuepuka hali hii ya kukataliwa na watu.
20. Jua katika nafasi ya kuwa na watu wengi wapya katika mtandao wa watu kuna makundi mawili ya watu. Wapo wale ambao wanapenda kuwa na watu muda mwingi na huitwa “Extroverts”. Watu hawa hujenga kirahisi mahusiano na watu wapya. Kundi la pili ni “Introverts” ambao huonekana wasiopenda sana kujichanganya katika makundi ya watu wengi na muda mwingi wapo katika kuwa peke yao. Kundi hili wakati mwingine hupata shida kuwa na mtandao mkubwa wa watu.
21. Tengeneza ujumbe wako wa pekee na watu wakutambue kwa hilo. Ujumbe unaobeba ni katika kile ulichokuwa tayari kukifanya na watu wameshakupa lebo hiyo. Wewe ni mwandishi, mwimbaji, mpigapicha, mfanyabiashara. Usisite kutambulisha unachokifanya ukiwa na watu mbalimbali. Huo utakuwa mwanzo wa kufungua milango ya watu wapya.
22. Haitoshi tu pekee umekutana na watu wapya katika tukio la kujenga mtandao wa watu “networking events”. Una nafasi ya kulea mahusiano hayo ili yawe na faida. Watu wengi tunakosea pale ambapo tunachukua nambari za watu na kuzijaza katika simu ila hatuendelezi mazungumzo nao mara baada ya tukio la kuonana nao. Jipe nafasi ya kuendeleza mazungumzo mara kwa mara na hili linakuza mahusiano na watu vizuri na mahusiano kuwa na faida au mtaji wa baadaye.
23. Katika simu yako utagundua leo kuwa kila mtu uliyempa nafasi ya kumhifadhi mawasiliano yake ukiangalia katika jicho la kina ni fursa ya pekee ya kukusaidia kukuunganisha na wateja wengine wa kuhitaji bidhaa au huduma yako. Zoezi kubwa la kufanya ni kujitahidi kuwa na taarifa nyingine za watu uloweka katika simu wanajishughulisha na nini, wanauza nini na wanatoa huduma gani. Isiishe kutunza tu namba ya mtu na ukakosa taarifa za biashara gani anafanya. Pengine unateseka kupata bidhaa au huduma fulani kumbe una hazina ya mawasiliano ya nambari za watu katika simu yako.
24. Mafanikio ya kukutana na watu wapya na ukafaidika na uwepo wa watu hao katika maisha yako, upo katika kujua mahitaji ya hao watu, wanachokipambania maishani na wewe kuwa sehemu kwa namna moja kuwasadia kuvuka hapo.
25. Jitahidi kuwa sehemu ya kushawishi wengine namna wanavyofikiri na kutenda kwa kushirikisha mambo yaliyo na manufaa kwao. Watu wengi wanapenda kuwa na watu ambao wana ushawishi mkubwa juu ya maisha yao. Iwe ni katika kufikiri au kutenda.
26. Yasimamie mahusiano ulojijengea na mtandao mpya wa watu. Endeleza mazungumzo nao, shiriki katika lile unaloweza kusaidia watu waliopo katika mtandao wako. Pongeza na toa pole pale ambapo watu waliopo katika mtandao wako wamekutana na nyakati za furaha au huzuni.
27. Njia nyingine nzuri ya kukuza mtandao mpya wa watu ni kuwa “Mtazamaji”. Tazama yanayoendelea katika mitandao, magazeti, Tv, majarida, Radio. Lengo ni kuangalia majina au mambo gani hutajwa mara kwa mara katika hayo maeneo. Kufuatilia hili linakupa kukua zaidi katika kupata watu wapya au kujua watu ulonao wanafanya vitu gani. Unaweza kuona kazi zao watu unaowajua iwe kwa Tv au magazeti. Usiwe mzito kuwatafuta na kuwapongeza au kuwapigia simu au kuwaandikia na kuwapongeza.
28. Umuhimu wa kuwa na mtandao wa watu unaendelea kuwa mkondo wa kupata mawazo mapya na inatumika kama nyenzo rahisi kufanikiwa.
29. Neno kubwa nalovutiwa na mwandishi ni pale anaposema licha utatumia mtandao wa watu ulonao katika kutafuta kazi, kutafuta taarifa, tafiti au kupata mawasiliano ya mtu binafsi bali ni njia kubwa ya kuongeza mduara wa ushawishi maishani mwako.
Huu uchambuzi umenifungua vitu vingi ambavyo awali sikuvijua kuhusu mambo yahusuyo kukutana na watu wapya, cha kufanya unapokuwa na watu wapya na namna ya kutunza mahusiano ya watu wapya. Naamini kitakusaidia na Wewe kujua pa kurekebisha na pakuongeza nguvu zaidi.
Kwa maswali, maoni na mrejesho usisite kufanya kwa njia utakayopenda kati ya kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi, whatsapp au njia ya barua pepe.
Malenga wa Ubena
Mchambuzi wa Vitabu
+255 676 559 211
Nyuma ya Pazia ya Uchambuzi huu.
Kazi imekamilika kwa masaa mawili na dakika 10. Hii ni pamoja na kuhariri tena