Wengi wetu tumetokea familia zinazojihusisha na kilimo au tunafanya kilimo. Hivyo tunaelewa vizuri sana kuhusu magugu yanapokuwa shambani.
Magugu huwa yanazuia mazao yaliyopandwa yasipate virutubisho na kukua vizuri, kwa sababu yananyonya rasilimali nyingi za ardhi.
Ukitaka kuondoa magugu shambani, kuna njia mbili unaweza kutumia.
Njia ya kwanza ni kuyafyeka au kuyakata, ni njia ya haraka, isiyohitaji kazi kubwa, lakini wote tunajua matokeo yake, mizizi ya magugu inakuwa imebaki na hivyo kuota tena kirahisi.
Njia ya pili ni kuyang’oa kabisa magugu hayo, kuondoa kabisa mizizi yake, hii ni kazi kubwa inayohitaji muda na juhudi, lakini matokeo yake huwa yanadumu, magugu hayarudi haraka.
Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye maisha yako ya mafanikio, kuna tabia za aina mbili, zinazokusaidia kufanikiwa na zinazokuzuia kufanikiwa.
Tabia zinazokusaidia kufanikiwa ndiyo mazao yako na zile zinazokuzuia kufanikiwa ndiyo magugu.
Ili ufanikiwe, lazima upalilie tabia za mafanikio na kuondoa magugu ambayo ni tabia zinazokuzuia kufanikiwa.
Wengi wamekuwa wanahangaika na tabia hizo kwa njia isiyo sahihi, badala ya kwenda kwenye mzizi wa tabia na kuung’oa, wanafyeka. Kinachotokea ni tabia hizo zinaendelea kujirudia mara kwa mara na kuwa kikwazo kwa mtu kufanikiwa.
Kaa chini na uorodheshe tabia zote ulizonazo kwa kuzigawa makundi mawili, zinazokusaidia kufanikiwa na zinazokuzuia kufanikiwa. Kwa zinazokusaidia kufanikiwa jua jinsi ya kuzichochea zaidi. Na kwa zinazokuzuia kufanikiwa jua mzizi wake kisha zing’oe kabisa na siyo kuzifyeka tu.
Kuanzia kwenye fedha, afya, mahusiano, kazi na maeneo mengine ya maisha yako, angalia ni tabia gani zimekuwa zinakukwamisha, kisha angalia tabia hizo zinatokana na nini, yaani chanzo chake hasa. Kisha ingia kwenye chanzo hicho na kitatue.
Mfano unaweza kugundua kwamba moja ya tabia zinazokurudisha nyuma kwenye kazi ni kupoteza muda kwenye mambo yasiyo muhimu. Unaweza kuhangaika sana na yale yanayokupotezea muda, lakini bado yakaendelea kukukwamisha. Ni muhimu kuchimba mzizi hasa, ambapo kwa upande wa kazi unaweza kugundua hupendi kazi unayoifanya au hujiamini kwenye kazi hiyo, hivyo unatumia muda mwingi kutoroka kazi. Kama ukijua hivyo na ukatafuta kitu unachokipenda kwenye kazi yako na kujijengea kujiamini zaidi, utajikuta unapata msukumo wa kufanya kazi kuliko kupoteza muda.
Wakati mwingine unaingia kwenye tabia zinazokuzuia kufanikiwa pale unapokuwa umechoka, una njaa, una hasira au una upweke. Tabia kama za ulevi na matumizi mabaya ya fedha zinachochewa sana na hali ambayo mtu anakuwa anapitia. Ni muhimu kuchunguza ni wakati gani umekuwa unarudia tabia zinazokuwa kikwazo kwako na kuwa makini katika nyakati hizo.
Chochote kilicho rahisi kufanya, hakijawahi kuzalisha matokeo makubwa na yenye thamani. Hivyo kwenye kujijengea tabia nzuri na kuvunja tabia mbaya, nenda kwenye mzizi na kuung’oa badala ya kufyeka tu kwa juu.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Chochote kilicho rahisi kufanya, hakijawahi kuzalisha matokeo makubwa na yenye thamanj.
Asante sana Kocha.
LikeLike
Kabisa
LikeLike