“Change your life today. Don’t gamble on the future, act now, without delay.” — Simone de Beauvoir
Chochote unachopanga kufanya kwenye maisha yako, kifanye sasa.
Kwa sababu huu ndiyo wakati pekee ambao una uhakika nao kwenye maisha yako.
Hutapata wakati mwingine kama sasa.
Ni rahisi kujiambia utafanya kesho,
Lakini kumbuka kesho huwa haifiki, kwa sababu na kesho ina kesho yake pia.
Lakini pia kujiambia utafanya kesho ni kucheza kamari,
Kwa sababu huna uhakika wowote kuhusu kesho, uhakika pekee ulionao ni sasa, hivyo utumie huo vizuri.
Litakuwa jambo la kushangaza kama utatumia muda huu ulio na uhakika nao kufanya yasiyo muhimu huku yale muhimu ukiyapeleka kwenye muda usiokuwa na uhakika nao.
Ni sawa na kucheza kamari ambayo umeambiwa timu A ina uhakika wa kuishinda timu B na sababu zenye mashiko umepewa, lakini bado dau lako ukaweka kwenye timu B kushinda.
Hiyo ndiyo kamari unayoicheza kila wakati unapoahirisha yale ambayo ungeweza kufanya kwenye wakati husika na kujiambia utafanya wakati ujao.
Achana na hiyo kamari sasa, tambua muda pekee wa uhakika ulionao ni sasa, huna muda mwingine wa uhakika zaidi ya sasa.
Hivyo yale yote muhimu, yafanyike sasa.
#NidhamuUadilifuKujituma
#AfyaUtajiriHekima
#KaziUpendoHuduma
Ukurasa wa kusoma leo ni kuhusu njaa, hasira, upweke na uchovu, soma hapa; http://www.kisimachamaarifa.co.tz/2020/11/30/2161
Rafiki yako anayekupenda sana,
Kocha Dr Makirita Amani